Afisa Elimu sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mwl. Patrick Haule ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule tano mpya kupitia programu ya uboreshaji wa Elimu Sekondari (SEQUIP).
Akizungumza ofisini kwake mjini Tunduru Afisa Elimu sekondari katika Wilaya ya Tunduru Mwl. Patrick Haule amesema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa SEQUIP kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali ya awamu ya sita ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 1.5 za ujenzi wa sekondari tatu mpya za kata ya Nakayaya, Majimaji na Lukumbule.
Shule zote za awamu ya kwanza ya programu hii zimekamilika na zimechukuwa wanafunzi wa kidato cha kwanza zaidi ya 500 katika shule zote tatu kwa mwaka huu.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Elimu Sekondari imepokea tena zaidi ya bilioni 1 kutoka serikali kupitia programu ya SEQUIP, ambapo shule mbili mpya toka kata ya Tinginya na Tuwemacho zitajengwa.
“Wanafunzi walikuwa wakitembea umbali zaidi ya kilomita 15 hadi 20 kutoka kata moja kwenda kusoma kata nyingine, hali iliyokuwa ilipelekea kuwepo kwa utoro mkubwa ambao ulisababisha wanafunzi wengi kuacha shule.”Alisema
Shule hizi za sekondari kupitia programu ya SEQUIP zitajengwa karibu na maeneo ya kuishi ili kuwawezesha wanafunzi kufika shule kwa wakati.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda,Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
23/08/2023.
WAKULIMA wa Mbaazi Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma wameingiza zaidi ya shilingi bilioni 1.69 baada ya kuuza Kilo 839,940 za mbaazi katika Mnada wa kwanza Msimu wa mwaka 2022/2023.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Oparesheni wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) Bw. Marcelino Mrope wakati akizungumza na Wanahabari ofisini kwake Mjini Tunduru.Bw, Mrope amesema TAMCU katika msimu wa Mwaka 2023/2024 imejiwekea malengo ya kukusanya Mbaazi Kilo 5,350,788 na kwamba katika msimu huu Chama kimeagiza viroba 130,000 kwa ajili ya kuhifadhia Mbaazi.
Hata hivyo, amesema kuwa ukusanyaji wa Mbaazi katika msimu wa 2022/2023 uliendelea kuuzwa kwa mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ambapo jumla ya Minada sita ilifanyika na Kilo 3, 035,692 ziliuzwa na kuwaingizia Wakulima zaidi shilingi bilioni 2.6.
“ukusanyaji wa zao la Mbaazi umepungua kidogo kutoka kilo 4,111,845 msimu wa mwaka 2021/2022 hadi kilo 3,035,692 msimu wa mwaka 2022/2023 ambapo ni sawa na anguko la asilimia 26.17 la ukusanyaji katika mauzo”, alisema.
Mnada wa pili wa zao la Mbaazi Wilayani Tunduru unatarajia kufanyika katika kijiji cha Msinji Agosti 24, 20
Imeandaliwa na Orpa Kijanda,Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
BILIONI 1.2 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA AFYA TUNDURU
Serikali ya awamu ya sita imetoa bilioni 1.2 kuboresha miundombinu ya hospitali kongwe iliyoanzishwa mwaka 1930 wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma.
Mganga mfawidhi wa hospital ya wilaya ya Tunduru, Daktari Athumani Mkonoumo amesema wamepokea shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya hospitali hiyo ambayo inajenga maabara mpya, Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na chumba cha upasuaji.
Amesema Serikali pia imetoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo ya wagonjwa wa Dharura (EMD), na kwamba limekamilika na kuanza kutoa huduma za dharura tangu Juni mwaka huu.
Vilevile, hospitali imepokea vifaa vya matibabu katika jengo hilo la dharura (EMD), vifaa hivi ni pamoja na Mashine ya X-Ray, Utrasound na mashine za kusaidia kupumua pamoja mitungi ya gesi ambapo hadi sasa wagonjwa zaidi ya 86 wamefanikiwa kupatiwa huduma zinazotolewa na EMD.
“Itatusaidia sana kutoa huduma bora na stahiki kwa sababu hatutokua na changamoto kubwa ya vifaa na miundombinu sahihi ya kutoa hizo huduma”. Alisema.
Ukarabati huu mkubwa wa hospitali utapunguza idadi kubwa ya wagonjwa kupewa rufaa ya kwenda kupata huduma nje ya wilaya.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda,Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
22/08/2023.
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.