Wanavikundi vya wajasiriamali na wafanyabiashara katika Halmashauri ya wilaya ya Tunduru ambao wamekidhi vigezo vya kupata mkopo wa asilimia kumi wapokea mafunzo ya mwisho. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 27.02.2025 katika ukumbi wa klasta Mlingoti.
Mafunzo haya yanalenga kuwaandaa wanavikundi hao ili waweze kutumia mikopo hiyo kwa ufanisi na kufikia malengo yao ya kukuza biashara zao. Mada zilizotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na, Usimamizi wa fedha, Uandishi wa mipango ya biashara, Mbinu mbalimbali za kibiashara, na Umuhimu wa kurejesha mikopo kwa wakati
Akizungumza katika mafunzo hayo Bi. Jeceline Mganga, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, aliwasihi wanufaika hao kuwa mabalozi wazuri na kuwasisitiza kutumia fedha hizo katika miradi au shughuli walizopanga ili ziweze kuwaletea faida na kuwawezesha kurejesha bila usumbufu
“Unaporejesha kwa wakati ndio unajiongezea sifa ya kukopa Zaidi” alisema Bi Jeceline. “Mikopo hii haina riba, hivyo tujitahidi kuitumia vizuri ili iwanufaishe”
Aidha, Baada ya mafunzo, wanufaika walitakiwa kusaini mikataba, kuashiria kukamilika kwa hatua muhimu katika kupata mikopo hiyo. Zoezi hili lilisimamiwa na Mwanasheria wa Halmashauri Bi.Mwanaharusi Chiutila.
Mafunzo haya muhimu yanawapa wajasiriamali na wafanyabiashara elimu ya jinsi ya kutumia mikopo hiyo ili kuweza kuelewa jinsi ya kutumia mikopo hiyo katika kuleta maendeleo na ufanisi katika biashara zao. Pia mafunzo hayo yanawawezesha wajasiriamali kutambua wajibu wao katika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Lengo kuu la mikopo hii ni kuwawezesha wananchi wa Tunduru kujikwamua kiuchumi na kuinua biashara zao. Mikopo hii inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza kipato cha wananchi, kukuza ajira, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika wilaya hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.