HISTORIA YA WILAYA YA TUNDURU
Wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa wilaya sita (6) za Mkoa wa Ruvuma. Wilaya hii ilianzishwa mwaka 1905 kipindi cha utawala wa ukoloni ambapo serikali ya Ujerumani ilijenga boma katika eneo la Kadewele karibu na lilipo jengo la Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa sasa.
UKUBWA WA WILAYA NA MAENEO YA KIUTAWALA
Wilaya ya Tunduru ina ukubwa wa kilometa za mraba 18,778. Pia, Wilaya ina Tarafa 7, Kata 39, Vijiji 157, Vitongoji 1,166 na Majimbo 2 ya Uchaguzi (Tunduru Kaskazini na Tunduru Kusini). Wilaya ina Waheshimiwa Madiwani 53 (Wakuchaguliwa 39, Viti Maalumu 14), na Waheshimiwa Wabunge 3 (Wakuchaguliwa 2 na Viti Maalum 1).
Wilaya ya Tunduru ipo kati ya nyuzi 36° 30’ na 38° Longitudo kuelekea upande wa Mashariki, nyuzi 10° 15’ na 11° 45’ Latitudo Kusini ya Ikweta.
IDADI YA WATU
Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti, 2012 idadi ya wakazi ilikuwa 298,279 kati yao Wanaume ni 143,660 (48.2%) na Wanawake ni 154,619 (51.8%). Mwaka 2016, Wilaya inakadiriwa kuwa na wakazi 331,821 kati yao Wanaume ni 159,815 na Wanawake ni 172,006. Wastani wa ongezeko la wakazi katika Wilaya ya Tunduru ni asilimia 2.7 kwa mwaka.
HALI YA HEWA
Hali ya hewa ni ya joto la wastani wa nyuzijoto 25°c linalofaa kwa ustawishaji wa mazao mbalimbali. Wastani wa mvua ni milimita 960 kwa mwaka ambapo mvua hunyesha kuanzia mwishoni mwa mwezi Novemba hadi Aprili. Aina ya uoto ni miombo. Hali ya udongo ni mchanga na mfinyanzi kwenye maeneo ya mabonde. Asilimia 30 ya vijiji ndani ya wilaya vina mito isiyokauka kwa mwaka mzima. Wilaya ya Tunduru ina mwinuko wa kati ya meta 200 na 500 kutoka usawa wa bahari na hali ya nchi ni ya tambarare na vilima upande wa Kusini Magharibi.
SHUGHULI ZA KIUCHUMI
wilaya ya Tunduru ni wilaya ambayo shughuli kubwa za kiuchumi ni kilimo cha zao la biashara la korosho ambayo hulimwa karibu katika maeneo yote ya wilaya, pia watu wa Tunduru wanalima mazao mengine kama mpunga, mbaazi, choroko, kunde,ufuta na karanga.
wilaya ya Tunduru ina vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo ni mbuga ya wanyama selous, mapori ya akiba ya sasawala na muhuwesi, masalia ya majengo ya wapigania uhuru wa msumbiji kupitia chama cha Frelimo, makaburi ya viongozi wa kimila, Miti inayogeuka kuwa mawe, mapango ya ajabu na nyayo za wanyama katika mwamba vyote hivi ni sehemu ya utalii na vinapatikana katika wilaya ya Tunduru pekee.
shuguli nyingine za uchumi zinazofanywa na wananchi wa wilaya ya tunduru ni shughuli za biashara, ufugaji wa nyuki, kuku, samaki, mbuzi na ngombe. pia wanafanya biashara za aina mbalimbali katika mazingira yao.
MAKABILA.
Wilaya ya Tunduru wakazi wake ni kabila kubwa la wayao, na makabila mengine ni ngoni, makua, na wandendeule.
Utamaduni
kabila la wayao kama zilivyo jamii nyingi za mikoa ya kusini wakati wa mavuno wanakuwa na ngoma, na baada ya mavuno wengi wao huandaa sherehe za jadi maafu kama unyago. ngoma hii huwa na lengo la kuwafundisha mabinti namna ya kukabiliana na changamoto za maisha hasa katika ndoa. kuna aina mbali mbali za ngoma kama mabega, mganda nk.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.