Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru leo imezindua rasmi Bodi ya mpya ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (TUUWASA). Uzinduzi huo uliofanyika leo, uliendana na miongozo ya mamlaka za maji katika miji midogo na makao makuu ya wilaya, ambapo bodi hiyo inaundwa na wajumbe saba wenye dhamana ya kusimamia masuala ya maji na usafi wa mazingira katika wilaya hiyo.
Pichani (aliyesimama) ni Mkurugenzi TUUWASA Mhandisi.Cuthbert Richard Kiwia
Uteuzi huu wa bodi mpya ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira umefanywa na Waziri mwenye dhamana katika serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), utadumu kwa miaka mitatu (3) kuanzia tarehe 12/02/2025 hadi tarehe 12/02/2028
Bodi hii itakayofanya kazi kwa miaka mitatu(3) inaundwa na Bwn. Jonathani A.Haule ambaye ni Mwenyekiti na Mhandisi.Cuthbert Richard Kiwia ni Katibu, Wajumbe wakiwa ni Ndg.Chiza Cyprian Marando, Mhe.Hairu Hemedi Mussa, Bi.Fatuma A.Makumbusya, Bi.Marcela V.Mapunda na Adv.Kaukuya Yusuph Kaukuya.
Pichani ni Bwn. Jonathani A.Haule ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Chacha aliwasisitiza wajumbe wa bodi hiyo kusimamia kwa umakini rasilimali za maji, miundombinu, na pia kufanya kazi kwa ushirikiano na mamlaka nyingine zilizopo ili kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza. Alikiri kuwa upatikanaji wa maji kwa sasa hautoshi kulingana na mahitaji ya wananchi, akisisitiza kuwa suala la maji linagusa uhai wa kila mmoja.
"Hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa haitoshi kabisa ukilinganisha na mahitaji halisi, upo umuhimu wa usimamizi wa uwiano wa rasilimali za maji ili kuhakikisha kuwa maji hayawi kikwazo katika maendeleo ya jamii yetu " alizungumza Mhe. Chacha kwa msisitizo. "Tunapozungumzia suala la maji, tunagusa uhai wetu moja kwa moja, hivyo suala la kuendeleza na kusimamia rasilimali hii ili itumike katika kizazi cha sasa na cha baadae."
Aidha, Bodi hii mpya yenye jukumu kubwa la kuishauri serikali kupitia wizara ya maji namna bora ya kuboresha huduma ya bora ya maji katk mazingira yaliyopo inatarajiwa kuwa chachu katika kuhakikisha wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru wanapata huduma ya maji kwa ukamilifu. Mheshimiwa Chacha alimpongeza pia Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Tunduru (TUUWASA) Mhandisi.Cuthbert Richard Kiwia kwa kazi nzuri anayoifanya, akibainisha kuwa hakujakuwa na malalamiko yoyote hadi sasa, na mipango mipya kabambe ya kuboresha huduma inaendelea kuandaliwa kwa manufaa ya wananchi.
Hii ni bodi ya kwanza ya wakurugenzi kuundwa katika wilaya ya Tunduru kwa ajili ya mamlaka ya maji. Mheshimiwa Chacha aliongeza kwa kusema, "Wadau wa kwanza wa utumiaji wa maji ni wananchi wenyewe," alihimiza Mhe. Chacha. "Hakikisheni rasilimali maji zinatunzwa kwa kila hali. Ikiwezekana, undeni sheria ndogondogo ambazo zitawasaidia kuendesha bodi hii kwa ufanisi."
Uzinduzi huu unaashiria hatua muhimu katika jitihada za kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Tunduru, huku ushirikiano kati ya bodi, mamlaka zilizopo, na wananchi ukiwa ni nguzo muhimu ya mafanikio.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.