Leo, tarehe 27 Machi 2025, kikao muhimu cha huduma za afya ya msingi kilifanyika wilayani Tunduru. Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa kujadili na kuweka mikakati ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Mpox. Kikao hicho kiliwakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu wa afya, na wadau mbalimbali kutoka ndani ya wilaya.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru, Ndugu Milongo Sanga, alimwakilisha mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mheshimiwa Simon Chacha, alitoa wito kwa wananchi kutozua taharuki. Alisisitiza kuwa hadi sasa, hakuna mgonjwa wa Mpox aliyeripotiwa wilayani humo. Alihimiza uzingatiaji wa masharti na maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na ugonjwa huo.
Pichani ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru, Ndugu Milongo Sanga
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Grace A. Mhagama, alisisitiza kuwa wote waliohudhuria kikao hicho wawe mabarozi wazuri ili kila mmoja achukue tahadhari juu ya ugonjwa huu. Aliongeza kwa kuzungumza kwamba kila mwananchi ana jukumu la kuelimisha wengine kuhusu dalili, njia za maambukizi na namna ya kujikinga na ya ugonjwa wa Mpox.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi, Daktari Athumani Mkonoumo, katika mada yake, alielezea dalili za ugonjwa huo, namna unavyoambukizwa na jinsi ya kujikinga, na pia alibainisha kuwa Mpox ni ugonjwa ambao hadi sasa hauna dawa ya moja kwa moja. Alifafanua kuwa wagonjwa wanaopatikana na ugonjwa huo hupewa matibabu kulingana na dalili wanazozionesha, huku wakitengwa na watu wengine ili kuzuia maambukizi.
Pichani ni Mganga Mfawidhi wa wilaya ya Tunduru, Daktari Athumani Mkonoumo
Afisa Afya wa Wilaya Bwana. Ayubu Majumbewima alieleza kuhusu hali ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Mpox tangu Wizara ya Afya ilipotoa tangazo la uwepo wa ugonjwa huu nchini. Alisema Halmashauri ya Wilaya imechukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kupitia kliniki za akina mama, siku za lishe, mashuleni, mikutano ya hadhara, na vijiwe. Pia, mabango yenye taarifa kuhusu ugonjwa huo yamesambazwa na kubandikwa, na elimu inatolewa kupitia redio.
Pichani ni Afisa Afya wa Wilaya Bwana. Ayubu Majumbewima.
Aidha, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imetenga jengo maalum kwa ajili ya kuwatenga wagonjwa watakaobainika kuwa na dalili za Mpox. Pia, gari limetayarishwa kwa ajili ya usafiri wa wataalamu wa afya na wagonjwa.
Viongozi wa afya walisisitiza ushirikiano kutoka kwa jamii ili kuhakikisha ufanisi katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. Ushirikiano huu unajumuisha kutoa taarifa sahihi, kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya, na kuepuka tabia zinazoweza kuhatarisha afya.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.