Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Simon Chacha amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Misechela na kata ya Namasakata. Lengo la mkutano huo lilikuwa kusikiliza kero za wananchi na kutatua.
Katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya alionya wafugaji holela wanaokaidi agizo la kupeleka mifugo yao kwenye vitalu vilivyotengwa. Aliwaagiza waache kupeleka mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na badala yake wafuate sheria kwa kuweka mifugo yao kwenye vitalu.
Mhe. Chacha pia aliwaasa wakulima na wafugaji kukaa pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto zao kwa amani badala ya migogoro. Alisema kuwa ana jukumu la kuhakikisha usalama wa wananchi wote wa Tunduru, lakini akaomba ushirikiano kutoka kwa jamii ili kuishi kwa amani na utulivu.
Pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Simon Chacha akizungumza na wananchi.
Mbali na hilo, Mhe. Chacha alisisitiza pia juu ya ulinzi wa watu wenye ulemavu wa ngozi. Aliagiza kutokuruhusu kufanyiwa vitendo vya ukatili, na akasema, "ninaomba tuwalinde watoto hawa kwa umoja wetu. Jamii inayomzunguka ndio mlezi wa kwanza. Tutambue kuwa wana haki zote za kibinadamu. Msiwafanyie vitendo vya kikatili wala kuwaficha ndani. Toeni taarifa ili tuhakikishe wanapata ulinzi."
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Tunduru, SSP.Shadrack Msasa, alieleza kuwa tayari wameanza kukusanya taarifa za watoto wenye ulemavu wa ngozi wote waliopo katika Wilaya ya Tunduru. Aliwaagiza Watendaji na wenyeviti wa vijiji zote kushirikiana katika kukamilisha orodha ya watoto hawa na kuwaweka kwenye kanzidata kwa ajili ya ulinzi bora zaidi.
Pichani ni Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Tunduru, SSP.Shadrack Msasa
Mkutano huo ulifanyika kwa amani na utulivu, na wananchi walionyesha shukrani kwa Mkuu wa Wilaya ambaye pia alijitambulisha kwao, kusikiliza kero zao na kuzitatua.
Imetolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,
Orpa Kijanda,
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.