Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru leo tarehe 15 Februari 2026 limefanya Mkutano Maalum wa kupitia Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, kufanya mapitio ya utekelezaji wa nusu mwaka wa fedha 2025/2026 (Julai–Desemba 2025) pamoja na kuidhinisha makadirio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Klasta na kuongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mhe.Sefu Hassan Dauda. Katika mkutano huo, Baraza la Madiwani limepokea, kujadili na kupitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 yenye jumla ya Shilingi 55,049,778,000.00.

Kati ya fedha hizo, Shilingi 38,027,851,400.00 sawa na asilimia 60 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu, huku Shilingi 17,021,926,600.00 sawa na asilimia 40 zikitarajiwa kupatikana kupitia makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Bajeti hiyo inaonesha ongezeko la asilimia 2.71, linalotokana na kuongezeka kwa makisio ya mapato ya ndani kutoka Shilingi 8,998,423,000.00 mwaka wa fedha 2025/2026 hadi kufikia Shilingi 10,497,251,000.00 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha rasimu ya Mpango na Bajeti kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Mkuu wa Idara ya Mipango, Bosco Mwingira, amesema kuwa Halmashauri imekadiria kukusanya Shilingi 10,497,251,000.00 kutoka mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Kati ya fedha hizo, Shilingi 6,038,804,000.00 ni mapato yasiyolindwa, huku Shilingi 4,458,447,000.00 yakitokana na mapato lindwa.

Aidha, kupitia mapato ya ndani na utekelezaji wa mipango mkakati ya Halmashauri, mojawapo ya vipaumbele vikuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ni kuimarisha sekta za huduma za jamii. Halmashauri imepanga kuajiri Walimu 100 wa kujitolea kwa mkataba kwa ajili ya Elimu ya Awali na Msingi, Watumishi 56 wa Sekta ya Afya, pamoja na Walimu 16 wa Mkataba, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.