Tunduru, Februari 16, 2026
Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Tunduru (DCC), kilichoongozwa na Mhe.Denis Masanja, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, kimefanyika leo Februari 16, 2026 katika ukumbi wa Skyway, kwa lengo la kupitia na kujadili rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Katika kikao hicho, wajumbe wa DCC walijadili kwa kina rasimu ya mpango na bajeti hiyo na hatimaye kuridhia kuipitisha, wakibainisha kuwa imezingatia vipaumbele vya maendeleo ya wananchi na mahitaji halisi ya Wilaya ya Tunduru.

Aidha, Kamati ilijadili na kuridhia mapendekezo ya kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru yenye ukubwa wa kilomita za mraba 18,778 kuwa Halmashauri mbili (2). Mchakato wa mgawanyo huo ulianza mwaka wa fedha 2018/2019, ukiwa na lengo kuu la kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi, ikizingatiwa kuwa ukubwa wa eneo la kiutawala umekuwa changamoto katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa ufanisi na kwa wakati.
Kwa sasa, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru inahudumia tarafa 7, kata 39, vijiji 157 na vitongoji 1,179. Wilaya hiyo pia ina majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Tunduru Kusini, inayojumuisha tarafa 3 za Namasakata, Nalasi na Lukumbule, pamoja na Tunduru Kaskazini yenye tarafa 4 za Matemanga, Mlingoti, Nakapanya na Nampungu.

Umuhimu wa kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru unatokana na sababu kadhaa ikiwemo ukubwa mkubwa wa eneo la kiutawala na mtawanyiko wa kijiografia, idadi kubwa ya watu, kata na vijiji ikilinganishwa na Halmashauri nyingine, pamoja na haja ya kuwa na mgawanyo bora wa rasilimali fedha na rasilimali nyingine kulingana na idadi ya watu na ukubwa wa maeneo husika. Hatua hiyo inalenga kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii, kuharakisha maendeleo ya wananchi na kuongeza ufanisi wa utendaji wa Serikali kwa ujumla.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa mipango na maamuzi yaliyofikiwa, kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.