Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Tunduru Mheshimiwa Hairu Mussa, imefanya ziara ya siku mbili ya kukagua miradi ya maendeleo ya miundombinu ya elimu na afya katika wilaya hiyo. Ziara hiyo ilifanyika tarehe 18 na 19 Mei 2024.
ziara hiyo pia iliambatana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru. Lengo la ziara hiyo lilikuwa kutathmini maendeleo ya miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokubalika.
Wakati wa ziara hiyo, kamati ilikagua miradi mbalimbali ya ujenzi wa shule, zahanati, na vituo vya afya katika kata mbalimbali za wilaya.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti Mussa aliwaagiza wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha inakamilika kwa wakati uliopangwa ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.
"Tumefurahishwa na maendeleo ya miradi hii," alisema Mwenyekiti Mussa. "Tunawaagiza wasimamizi wa miradi hii wahakikishe inakamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu. Tunataka wananchi wa Tunduru waanze kunufaika na miradi hii haraka iwezekanavyo."Alisema Mheshimiwa Mussa.
Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango pia walipongeza mwenendo wa ujenzi wa miradi hiyo na kuwataka wasimamizi wahakikishe kuwa inajengwa kwa uadilifu na kwa uwazi. Walisisitiza pia umuhimu wa ushirikiano kati ya kamati za ujenzi na wananchi katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa mafanikio.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru za kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa uwazi. Halmashauri inaamini kuwa miradi hii itaboresha maisha ya wananchi wa Tunduru kwa kiasi kikubwa
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.