Katika hatua kubwa ya kuimarisha sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa chakula, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeidhinisha kuanza kwa mradi mkubwa wa umwagiliaji katika Kijiji cha Nambarapi, Kata ya Masonya, Wilaya ya Tunduru. Mkandarasi aliyepewa dhamana ya kutekeleza mradi huu ataanza kazi tarehe 29.07.2024, na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18, kufikia tarehe 31 Desemba, 2025.
Makabidhiano ya mradi huu wenye thamani ya shilingi bilioni 6,314,477,066.00 baina ya Tume ya Taifa ya umwagiliaji kwa mkandarasi yamefanyika kwa sherehe za hadhara katika kijiji cha Nambarapi, zimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Simon Chacha, ambaye alikuwa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Pichani ni Mkandarasi akionyesha Hati aliyokabidhiwa
Katika hotuba yake Mhe. Chacha alisisitiza umuhimu wa mradi huu katika kukuza uchumi wa wilaya na kuboresha maisha ya wananchi. Na pia, alimsisitiza Mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huu kutekeleza kwa muda uliopangwa huku akizingatia ubora waliokubaliana na serikali wakati wa kupokea mkataba wa kazi.
“Mradi huu ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika sekta ya kilimo na kuboresha maisha ya wananchi, ni mradi ambao ukikamilika vyema hautakuwa na msimu, utafanya kazi kwa kipindi chote cha mwaka” alisema Mhe. Chacha “kuimarika kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja ndio kuimarisha uchumi wa taifa zima”.
Aidha, akielezea Mradi huu Msaidizi wa Mradi-Skimu ya Nambarapi, Mhandisi Lusia Chaula alisema, kazi zitakazofanywa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa banio na tuta, ujenzi wa mfereji mkuu, ujenzi wa mfereji wa upili, ujenzi wa mfereji wa matupio, ujenzi wa barabara za mashambani, ujenzi wa vivusha maji, na ujenzi wa ofisi ya mhandisi.
Akizungumza katika Mkutano huo Diwani wa Kata ya Masonya Mhe. Bwanali ameahidi atahakikisha kata yake inatoa ushirikiano mkubwa huku akisisitiza mkandarasi kuwapa kipaumbele wananchi wa kata hiyo katika kazi ambazo zitajitokeza ambazo wataona zinawafaa wanakijiji.
Pichani ni Diwani wa Kata ya Masonya Mhe. Bwanali
Imetolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,
Orpa Kijanda,
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.