Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe.Julius Mtatiro wakati akiongea na watumishi wa Idara ya Mifugo na Kilimo,watendaji wa Kata pamoja na maafisa Tarafa katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa klasta mapema wiki hii cha kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani Tunduru.
Akiongea katika ufunguzi wa kikao hicho Mhe.Julius Mtatiro alianza kwa kuwapongeza watendaji kwa utendaji kazi uliotukuka wa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika wilaya ya Tunduru ikiwa ni pamoja na kufunguka kwa barabara ya lami na kurahisha usafirishaji na uchukuzi.
Mkuu wa wilaya huyo alisema anapenda kufanya kazi na watu wanatoa taarifa zilizo sahihi na mashauriano “nendeni mkasome mjue majukumu yenu ni yapi usisubiri mpaka kuagizwa na mkuu wa idara yako ya kilimo au mifugo, siamini katika falsafa ya kuletewa taarifa ndio utekeleze majukumu yako”
Aidha katika kikao hicho aliweka mikakati ya utendaji kazi ambayo itaenda kutatua migogoro iliyopo kati ya wakulima na wafugaji, ikiwa ni pamona na mikataba ya vitalu kwenye maeneo tengefu iwe shirikishi kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa kata ili kuwa na nguvu ya kufanya maamuzi inapotokea hali ya kutokuelewana kati ya wakulima na wafugaji.
Maafisa kilimo na mifugo wa Kata waache kufanya kazi kwa mazoea, wengi wao wanasubiri kuagizwa na wakuu wa wao wa idara, aliwataka kuamka na kutafuta taarifa na kuwahudumia wananchi kwenye maeneo waliyopangiwa.
Halmashauri kupitia baraza la madiwani kutunga sheria ndogo mahusuano kwa ajili ya usimamizi wa mifugo ili itumike katika kupunguza migogoro, pia kuhuisha sheria ndogo za Halmshauri ambayo itatoa mwelekeo wa uendeshaji wa shughuli za wafugaji na wakulima katika hali ya Amani na usalama.
Serikali ipo katika hatua za kuhakikisha kuwa maeneo yote tengefu ya vitalu vya wafugaji miundombinu wezeshi inajengwa ili kupunguza ufugaji wa kuhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingi kutafuta malisho hasa wakati wa kiangazi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Tunduru Ndg Gasper Balyomi alipokea maelekezo hayo na kuwataka watendaji wote na maafisa waliopo katika ngazi ya kata kuwa makini na kushughulikia masuala yanayohusu migogoro ya wakulima na wafugaji kwani yanaweza kuleta maafa makubwa kwa jamii ya Tunduru.
Aidha aliwataka kuhakikisha kuwa wafugaji wanatekeleza masharti waliyopewa wakati wanapangiwa vitalu na endapo watakua wanakiuka utaratibu na sheria iliyowekwa basi wapigwe faini kulingana na sheria ya mazingira ya mwaka 2004, na ikifanyika hivyo wafugaji wataacha kuvunja sheria.
Vilevile alikema tabia ya watendaji kuruhusu wakulima na wafugaji kumaliza migogoro kienyeji iachwe mara moja na ifike mwisho kwani ndio linalochochea migogoro kuendelea kuwepo “suala la wakulima na wafugaji kumalizana kienyeji lifike mwisho, sheria izingatiwe, hii kuelewana iishe, mtu akifanya kosa apigwe faini kubwa”
Kwa upande wa kamanda wa polisi wilaya Livingstone Nicholausi Mwakasanga alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuhamasisha migogoro ya wakulima na wafugaji, akitaja baadhi ya maeneo ya sisi kwa sisi, kijiji cha Angalia, na Mwenge imechangiwa kwa kiwango kikubwa na viongozi.
Hata hivyo waliaswa kuacha tabia ya kupenda kupokea zawadi ndogondogo ambazo zinawapelekea kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.