Chama cha Ushirika cha Msingi Mndichana (Mndichana AMCOS) kimewafuta uwanachama, wanachama watatu kutokana na utovu wa nidhamu na kutotimiza masharti ya chama, ikiwemo kutokuuzia mazao yao kwenye chama hicho.
Tukio hili lilitokea katika Mkutano Mkuu wa kawaida wa chama uliofanyika katika Kijiji cha Msinji, Kata ya Ligoma, lengo likiwa kujadili taarifa za chama kwa msimu wa 2023/2024.
Meneja Mkuu wa chama hicho, Bw. Hassani Bakari Makina, aliwasilisha changamoto zilizokikabili chama wakati wa msimu wa ukusanyaji korosho. Alisema wanachama watatu walishinikiza wakulima na wanachama wengine kutokuuzia mazao yao kwenye chama hicho na pia walihamasisha vurugu.
Bw. Makina alieleza kuwa kutokana na kutotimiza masharti ya chama na utovu wa nidhamu, bodi ya chama ilipendekeza kuwafukuza wanachama hao.
Afisa Ushirika, Ndg. Raymond Raphael, alifafanua kuwa kulingana na kanuni na masharti ya chama cha Mndichana, hatua zitachukuliwa dhidi ya watu wanaohusika na makosa hayo.
“Bodi imeleta mapendekezo kwenu wanachama, ninyi kama wamiliki wa chama mnatakiwa kufanya maamuzi kulingana na kanuni na Masharti ya chama chetu kama katiba inayotuongoza katika kusimamia chama chetu”
Wananchama walipiga kura kuamua kuhusu pendekezo la bodi, na kura nyingi zilionyesha wanachama hao wafutwe uwanachama.
Afisa Ushirika wa Wilaya ya Tunduru, Ndg. George N. Bisani, aliagiza bodi ya chama kuwaandikia barua wanachama hao wakielezwa makosa yaliyosababisha kufukuzwa kwao na kuwapa stahiki zao, kama vile hisa zao, ndani ya siku 90 tangu kufutwa kwa uwanachama wao.
Mkutano huo ulienda sambamba na Uchaguzi wa Bodi ya Chama hicho kama ilivyo taratibu ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika ya kufanyika kwa uchaguzi kwa vyama vyote vya Ushirika Nchini Tanzania.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.