“Warajisi Wasaidizi wa Mikoa na Maafisa Ushirika wa Halmashauri za Wilaya nchini wakutane na wadau wa vyama vya msingi vya zao la kahawa na wapitie upya tozo zilizo kwenye zao hilo, hayo ameyasema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kassimu Majaliwa katika ukumbi wa hazina jijini Dodoma”.
Aliyasema hayo wiki iliyopita (Jumamosi, Mei 19, 2018) wakati akizungumza na Warajisi Wasaidizi wa Ushirika wa Mikoa 25 na Maafisa Ushirika wa Halmashauri za Wilaya 140 zinazolima mazao makuu ya biashara yaani kahawa, chai, tumbaku, pamba na Korosho kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma ili kujadili namna bora ya kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na kufanya ufuatiliaji wa maagizo ambayo alikwishayatoa kwenye ziara zake mikoani.
Alisema tozo nyingi haziko kisheria bali zinawekwa na vyama vya msingi na zimelenga kuwanyonya wakulima badala ya kuwasaidia kuinua vipato vyao.
Akizungumzia kero ya tozo za mazao kwa wakulima, Waziri Mkuu alisema: “Kuna tozo nyingi zinazowekwa na vyama vya msingi na hazina uhalali wowote; tozo nyingine si za vyama vikuu, bali ni za AMCOS tu (vyama vya msingi)”
Akitoa mfano Waziri Mkuu alisema, “Wakati napitia nakala za baadhi ya vyama vya zao la kahawa, nimekuta chama kimoja cha Karagwe kimeweka sh. bilioni tano zikiwa ni gharama za kukagua maghala na ili kufidia gharama hizi, mkulima anakatwa sh. 260 kwa kilo moja. Nimejumlisha makato ya tozo zote nimepata sh.1,600 kwa kilo.”
Aidha waziri mkuu aliwataka warajisi pamoja na maafisa ushirika wilaya kufanya usimamizi wa mifumo ya masoko ili kupambana na wanunuzi nje ya mifumo iliyokusudiwa na serikali na kuwaibia wananchi.
“Kuna mifano ya wanunuzi wasio rasmi katika mkoa wa Kagera wanunuzi wa kahawa wasio rasmi wanaitwa butura, Moshi wanaitwa katakichwa, kwenye korosho wanaitwa kangomba na kwenye tumbaku wanaitwa vishada. Ninawasihi msikubali kuwe na uonevu, dhuluma na wizi kwa wakulima wetu,” alisisitiza.
Waziri mkuu aliwataka maafisa hao kuhakikisha kuwa wana takwimu sahihi ambazo zitaonesha idadi ya vyama vya msingi na wanachama wake, na kila mkulima analima ekari ngapi kwa msimu ili kusaidia na kurahisha usambazaji wa pembejeo za kilimo.
Aliendelea kutanabaisha kuwa serikali imeamua kuanza kuimarisha mazao manne ya biashara ili kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika kwa kupata matunda ya kazi zao, mazao hayo ni pamoja na Kahawa, Pamba, Chai,Korosho na Tumbaku.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini, Dk. Titus Kamani aliwataka maafisa hao wawe wabunifu na waondokane na utendaji wa mazoea ili wawasaidie wananchi kwa sababu ushirika ni silaha ya wanyonge na adui wa matajiri wanaowanyonya wakulima.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.