Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru inaendelea kutekeleza siku za lishe katika vijiji mbalimbali, hatua ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi hususan watoto na akina mama. Mpango huu unalenga kuhakikisha jamii inapata elimu ya lishe bora, huduma za afya ya msingi pamoja na ushauri kuhusu namna ya kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo yao kwa ajili ya kuimarisha afya.
Katika siku za lishe, wananchi wamekuwa wakipatiwa huduma za upimaji wa hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano, chanjo, elimu ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto wachanga, pamoja na mbinu sahihi za uandaaji wa vyakula vyenye mchanganyiko wa makundi matano ya chakula. Aidha, wananchi hufundishwa mbinu za kilimo cha bustani za mbogamboga ili kuongeza upatikanaji wa chakula chenye virutubisho kwa familia zao.
Kupitia utekelezaji wa programu hii, kumekuwepo na mafanikio makubwa ikiwemo kupungua kwa hali ya utapiamlo kwa watoto, kuongezeka kwa uelewa wa wazazi kuhusu malezi bora, pamoja na kuboreshwa kwa afya za akina mama wajawazito na wanaonyonyesha. Vilevile, jamii imehamasika zaidi kuhusu matumizi ya vyakula vya asili vinavyopatikana kwa urahisi majumbani mwao.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa siku za lishe, Afisa Lishe wa Wilaya ya Tunduru Ndg.Martine Kigosi, amewataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika siku hizi kwa kuwa ni fursa muhimu ya kuboresha afya za watoto na familia kwa ujumla.
Aidha, amesisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi wote vijijini na mijini, ili kufanikisha azma ya Serikali ya kupunguza tatizo la udumavu na kuimarisha afya za wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.