Mama Nasra Juma,Bi Zawadi na Bi Namsifu ni miongoni mwa wanawake wajasiri walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Unyonyeshaji Tunduru, ambapo walisimama kama mashuhuda na kuwahimiza kina mama wenzao. Kwa kujiamini na furaha, walieleza jinsi walivyonyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo bila kuwapatia maji wala chakula kingine.
Mama Nasra Juma, mkazi wa Tunduru, ni mmoja wa akina mama waliosimama na kutoa ushuhuda wa jinsi alivyonyonyesha watoto wake wawili maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo. Kwa tabasamu na uso wenye nuru, Mama Nasra Juma alisimulia safari yake: "Nilifuata ushauri wa wataalam wa afya na nikajizuia kabisa kumpa mtoto wangu maji, chai, au uji katika miezi sita ya kwanza. Watu walinishangaa, wengine walisema nitamtesa mtoto wangu, lakini nilisimama imara. Matokeo yake, mtoto wangu alikua na afya njema, hakuugua mara kwa mara, na ana akili timamu. Ninafurahi kuona ni mzima kabisa."

Ushuhuda huu uliungwa mkono na mama mwingine, Bi. Zawadi, ambaye alisisitiza umuhimu wa akina mama kuamini maziwa yao wenyewe. "Ninaona fahari sana ninapowaangalia watoto wangu wawili wakubwa ambao wote niliwanyonyesha kwa miezi sita ya kwanza bila kuwapa kingine. Hii inawezekana kabisa. Nawaomba wamama wenzangu msidanganyike na maneno ya mtaani. Kuwanyonyesha watoto wenu maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza si kuwatesa, bali ni kuwajengea afya imara kwa maisha yao yote,"
Akithibitisha kuwezekana kwa suala hili, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Bi. Namsifu alikazia msimamo wa serikali katika kuwezesha unyonyeshaji. Alifafanua kuwa licha ya shughuli nyingi za kiofisi, serikali imeweka sheria na miongozo inayomruhusu mama kupewa muda wa kutosha wa likizo ya uzazi na pia kupata muda wa kutosha kazini ili aweze kunyonyesha mtoto wake kwa miezi sita ya kwanza bila bughudha. Alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya kupata lishe bora kutoka kwa mama yake, na hivyo kujenga kizazi imara na chenye afya.

Ushuhuda huu ulitoa hamasa kubwa kwa kina mama wengine waliohudhuria hafla hiyo, kuwathibitishia kwamba unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita inawezekana na matokeo yake ni mazuri kwa afya ya watoto.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.