Wakulima wa ufuta wilayani Tunduru wameipongeza serikali kwa kusimamia soko la ufuta kufanyika katika mfumo wa ushindani wa bei katika msimu wa mwaka 2018/2019.
Mfumo huu umeleta tija sana kwa wakulima kwa kuongezeka kwa bei ya soko ukilinganisha na msimu uliopita ambapo ufuta ulinunuliwa kiholela bila kuwa na usimamizi na mkulima kupata bei ndogo ambayo haikuzidi shilingi 2500 kwa kilo ukilinganisha na msimu huu ambao bei yake ni zaidi ya shilingi 3000 kwa kilo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Tunduru Diwani wa Kata ya Marumba ambapo mnada wa pili ulifanyika katika Amcos ya Mtiti Mh.Msenga S.Msenga aliishukuru serikali kwa wakulima wa ufuta kulipwa kwa wakati fedha za zao la ufuta kwa kupata bei nzuri.
"tunaishukuru serikali kufanya usimamizi wa zao la ufuta, hapo awali zao hili liliuzwa kiholela sana na kwa bei ndogo hatukuwahi kuuza kwa bei kama za mwaka huu,mkulima anapata hadi shilingi 3000 kwa kilo,lakini pia wakulima wanalipwa kwa wakati kwani ndani ya wiki moja tuu baada ya mnada" alisema Diwani wa Marumba Msenga S.Msenga.
Afisa Ushirika wilaya George Bisani pamoja na ndg Imani Kalembo wakifungua sanduku la zabuni katika mnada wa pili wa Ufuta uliofanyika Marumba
Akizungumza na wananchi wakati wa mnada wa pili Katibu Tawala wilaya ya Tunduru Ndg Ghaibu Lingo alisema jumla ya kilo 478,393 ziliuzwa kwa bei ya shilingi 3066.17 ambapo jumla ufuta wenye thamani ya shilingi 1,466,833,829.00 uliuzwa kwa kampuni ya Alphakrust ltd.
Katibu Tawala alisema katika mnada wa kwanza wa ufunguzi wa uuzwaji wa zao la ufuta wilayani Tunduru uliofanyika katika Kata ya Lukumbule jumla ya kilo 239,368 ziliuzwa kwa bei ya shilingi 3080 ambapo jumla ya ufuta wenye thamani ya shilingi 737,253,440.00 ziliuzwa kwa kampuni ya Sunshine ltd.
Alitoa tahadhari kwa wakulima ambao wanafanya udanganifu kwa kuweka mchanga kwenye ufuta ili kuongeza uzito, serikali haitosita kumchukulia hatua kali za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.
Hata hivyo Mnada wa pili wa ufuta wilaya ya Tunduru ulifanyika katika Amcos ya Mtiti iliyopo kata ya Marumba wilayani Tunduru ambapo wanunuzi wapatao 8 walijitokeza kwa ajili ya kununua ufuta wa wakulima.
Mwisho.
Theresia Mallya
Imetolewa na Afisa Habari
Halmashauri ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.