Hayo yamesemwa na waziri wa Maji Makame Mbarawa akiwa katika ziara ya siku mbili wilayani Tunduru iliyoanza tarehe 20 hadi 21 octoba 2018, na kukagua miradi mitano ya maji inayoendelea kutekelezwa na ile iliyokamilika ya Mtina, Mbesa, Mradi wa Maji Tunduru Mjini, Nandembo na Matemanga.
Akisoma taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji wilaya ya Tunduru mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera alisema kuwa Halmashauri ya Tunduru ina jumla ya vijiji 157 lakini mpaka sasa vijiji vilivyofikiwa na mfumo wa huduma wa maji safi na salama ni 115 huku vijiji 38 vikiwa bado, pia ikiwa ni asilimia 64.4 ya wakazi waishio vijijini.
wananchi wa Kata ya Mtina wakimsikiliza Waziri wa Maji Mh. Makame Mbarawa ambaye hayupo katika picha akiwa kwenye ziara ya siku mbili ya ukaguzi wa miradi ya maji inayotekelezwa wilayani humo.
Aliendelea kusema kuwa wilaya kupitia program ya maendeleo ya sekta ya maji (WSDP) kuanzia mwaka 2012/2013 ilianza kutekeleza miradi katika vijiji 11 ambapo miradi minne 4 imekamilika, mitatu ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji na vijiji 4 maji hayakupatikana katika usanifu.
“miradi iliyokamilika inatoa huduma kwa jumla ya vijiji 12 vinanufaika na huduma ya maji safi na salama, vijiji hivyo ni Nandembo, Amka, Nangunguru, Lipepo, Chilundundu, Lukumbule,Mchesi, Amani, Meamtwaro, Mchengamoto na Chiungo” alisema Mkuu wa wilaya.
Kwa upande wa Waziri wa Maji Makame Mbarawa akiwa katika Ukaguzi wa miradi, alisema katika utekelezaji wa Ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2015/2020 serikali imedhamiria kutoa huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 95 kwenye miji ya mikoa, 90 miji ya wilaya na asilimia 85 katika vijiji ambapo alisema kwa sasa wilaya ya Tunduru imepiga hatua kutoka asilimia 53 na kufikia 66 mjini.
Mhandisi wa maji wilaya Ndg Bartolomeo Matwiga akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Maji Mbesa kwa Waziri wa Maji Makame Mbarawa.
Waziri Mbarawa alibaini changamoto kubwa katika miradi ya maji wilayani Tunduru ni vyanzo vya maji kukosa maji ya kutosha baada ya miradi kuanza kufanya kazi hali wakati wa usanifu vilionekana kuwa na maji, “hali hii inaweza kuchangiwa na uharibifu wa mazingira unaofanywa na wananchi kwa kukata miti, vilevile mabadiliko ya tabia ya nchi, niwaombe wananchi kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji ili miradi hii iwe endelevu”
Aidha aliwataka wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maji ya Mtina na Matemanga kukamilisha kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma ya maji na kuondoa adha ya wanawake kutembea umbali mkubwa kutafuta maji kwani ilani ya CCM inataka mwananchi asipate huduma ya maji kwa umbali usiozidi mita 400.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.