AFISA LISHE ATOA ELIMU YA LISHE KWA WAHUDUMU WA AFYA WILAYANI TUNDURU.
Katika juhudi za kuboresha huduma za afya na lishe katika jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imewapa mafunzo wahudumu wa afya kuhusu umuhimu wa lishe bora na uhusiano wake katika kuepuka udumavu na magonjwa yanayotokana na lishe duni. Mafunzo haya yameongozwa na Afisa Lishe Wilaya ya Tunduru ndg. Martini Kigosi. Aidha mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru siku ya tarehe 08/11/2024 na yalihusisha wauguzi, na wahudumu wengine wa afya.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Lishe Wilaya ya Tunduru Martini Kigosi alieleza kuwa lishe bora ni msingi muhimu katika kuzuia magonjwa mengi ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, na utapiamlo. Aliongeza kuwa wahudumu wa afya wanahitaji ujuzi wa kutosha kuhusu lishe ili waweze kutoa huduma bora na ushauri kwa wagonjwa wao na wananchi kiujumla hasa katika matibabu ya magonjwa yanayotokana na lishe duni.
Mafunzo yalijikita katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:
Jinsi ya kuwahudumia walengwa wa siku 1000 ambao ni kina Mama wajawazito, kina mama wanaonyonyesha na watoto chini ya miaka miwili kwa kuzingatia huduma bora za afya na lishe.
Jinsi ya kuwagundua watoto wenye utapiamlo mkali na matibabu ya watoto wenye utapiamlo mkali.
Jinsi ya kufanya tathmini ya hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano kwa kuwapima udumavu, ukondefu na uzito pungufu.
Ujazaji wa taarifa za afua za lishe ngazi ya kituo kwa usahihi na umuhimu wa kujaza taarifa kwa usahihi.
Bi.Leonatha Lutego, Maratibu huduma za afya ya Uzazi,Mama na Mtoto Wilayani Tunduru aliongeza kwa kusema kuwa wahudumu wa afya wanalo jukumu kubwa la kuwaelimisha wananchi kuhusu lishe bora na matumizi sahihi ya vyakula ili Kuondokana na tatizo udumavu.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za afya kwa jamii, na pia kuongeza ufanisi katika kudhibiti magonjwa ambayo yanatokana na matatizo ya lishe.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.