WACHIMBAJI wadogo wa madini wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kuangalia upya sheria inayotaka leseni zote za madini kufanya kazi katika eneo husika.
Wameeleza kuwa,sheria hiyo imesababisha Biashara ya Madini kudorola na baadhi ya wanunuzi wakubwa wa madini kukimbia na hivyo Serikali kukosa kodi na ushuru.
Wakizungumza jana, katika kikao cha kujadili juu ya mwenendo wa sekta ya madini na kero zinazo wakabili wadau wa Madini wilayani Tunduru wadau hao walisema, sheria hiyo inatengeneza mazingira kwa baadhi ya watu kutumia njia mbadala kutafuta soko na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Mathew Ngonyani alisema, sheria ya kuzuia madini kuuzwa katika eneo husika imesaidia sana kudhibiti udanganyifu na vitendo vya wizi,lakini haiwasaidii sana wachimbaji wadogo kwa kuwa baadhi ya madini yanayopatikana Tunduru soko lake liko nje ya Tunduru na mkoa wa Ruvuma.
Naye Mjumbe wa Chama cha wachimbaji Madini wilaya ya Tunduru Mohamed Rojas alisema, kuna aina 50 ya Madini yanayopatikana katika wilaya hiyo, hata hivyo aina 10 tu ambazo soko lake liko Tunduru na yanayobaki soko linapatikana mikoa mingine kama Arusha,Dar eslaam, na Maganzo mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wake, kuzuia kuuza madini hayo nje ya mkoa wa Ruvuma ni kuifanya kazi hiyo kuwa ngumu sana kwa Madalali(Mabroka) na wachimbaji wadogo ambao wanategea kazi hiyo kuendesha maisha yao ya kila siku ambapo wameiomba Serikali iangalie namna Bora ya kuruhusu Madalali na wachimbaji wadogo kwenda kuuza madini nje ya mkoa.
Rojas alisema,soko la madini lililopo Tunduru limekuwa na changamoto nyingi na kwa sasa sio rafiki tena, kwa kuwa Biashara hiyo inahitaji siri kubwa kwa muuzaji na mununuzi, kitendo cha kutumia chumba kimoja wanunuzi zaidi ya mmoja ina changia wachimbaji kushindwa kupata Bei nzuri.
Aidha,ameiomba Halmashauri ya wilaya ya Tunduru kuharakisha upatikanaji wa jengo Bora na lenye nafasi ili wanunuzi wakubwa wapate sehemu sahihi na Bora kwa ajili ya biashara hiyo.
Akijibu malalamiko hayo Katibu Tawala wa wilaya ya Tunduru Ghaib Lingo alisema, tayari Serikali imeshapa jengo kubwa ambalo litatumika kwa ajili ya ununuzi na uuzaji wa Madini yote yanayochimbwa katika wilaya hiyo.
Kwa mujibu wake,Serikali haijakataza wachimbaji na madalali kwenda kuuza madini nje,isipokuwa imewataka kufuata sheria ikiwemo kuwa na leseni inayoonesha kuwa uhalali wa madini hayo sambamba na vitambulisho vya wajasilimali kwa wachimbaji wadogo.
Pia, amewashukia wachimbaji wadogo na madalali hao kutokana na tabia yao ya kukwepa kulipa kodi na wengine kudiriki kuficha madini ambapo amesisitiza kuwa,serikali ya wilaya kwa kutumia kikosi kazi itahakikisha inawakamata na kuwachukulia hatua wale watakao kutwa wanauza madini nje ya vituo rasmi vilivyowekwa na Serikali.
Lingo ametoa siku kumi kwa wanunuzi wa madini,kuondoa haraka mabango ya matangazo yaliyowekwa kwenye nyumbani zao na kando kando ya Bara bara, kwa kuwa yanatumika sana kuuza na kununulia madini kinyume na utaratibu.
Amewataka wachimbaji wadogo,kuchangamkia fursa ya kutolewa vitambulisho vya wajasilimali ili kuepuka usumbufu kutoka kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) na vyombo vya dola pindi vitakavyoonza operesheni ya kuwasaka watu wanaokwepa kulipa kodi ambao mitaji yao inazidi Ml 4.
Kwa upande wake,mwakilishi kutoka ofisi ya Afisa Madini mkoa wa Ruvuma Getty Massawe alisema, Tume ya Madini italeta mtaalam ambaye atakuwa na kazi ya kufanya tathimini ya madeni yote na kujua thaman halisi, kabla ya kufika kwa mnunuzi hatua ambayo itasaidia kudhibiti udanganyifu na vitendo vya wizi wanavyofanyiwa wachimbaji wadogo.
Alisema, mchimbaji mdogo na dalali mwenye leseni yuko huru kuuza Madini popote ndani ya Tanzania kwa kutumia masoko yaliyopo ambapo amesisitiza kuwa uuzaji wowote wa madini nje ya vituo vilivyowekwa na Serikali ni kosa kubwa.
Naye Afisa Migodi wa Madini kutoka Ofisi ya Madini wilaya ya Tunduru Juma Kapera alisema, ofisi ya madini kwa kushirikiana na Chama cha Wachimbaji Madini Tunduru wapo katika hatua ya mwisho kupata jengo ambalo litatumika kama kituo kikuu cha kuuza na kununua madini.
MWISHO
|
|
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.