Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia Serikali ya Ujerumani (BMZ) limeanzisha mradi katika Wilaya ya Tunduru unaolenga kupunguza migongano ya binadamu na wanyamapori, hasa uvamizi wa tembo katika mashamba ya wakazi.
Kabla ya mradi huu, wakazi walikuwa wakipambana kulinda mazao yao kwa njia za jadi, kama vile kupiga kelele na kutupa mawe ili kuwafukuza tembo wanapoingia mashambani, lakini mara nyingi njia hizi hazikuwa na ufanisi. Hii ilisababisha hasara kubwa kwa mazao na hata kusababisha majeraha na vifo kwa baadhi ya watu.
Mmoja wa Askari wa Uhifadhi wa Kijiji (VGS), Bw. Yassin Mkwanda, anaelezea mafanikio ya mradi huo: "Tunashukuru GIZ kwa kutusaidia kujenga uzio wa pilipili kulinda mashamba yetu. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, tuna uwezo wa kukabiliana na wanyamapori hawa. Tunajaza chupa za maji na unga wa pilipili, ambao tembo wanachukia sana harufu yake, na kuziweka kwenye uzio wetu kwa kutumia kamba za mkonge."
Pichani ni Askari wa Uhifadhi wa Kijiji (VGS), Bw. Yassin Mkwanda
Hivi karibuni, vijana watatu kutoka kijiji cha Mbati wamehitimu mafunzo kutoka Kituo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Msingi ya Jamii (CBCTC) - Likuyu Sekamaganga kilichopo Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma. Vijana hawa wameanza kutumia maarifa waliyopata kuwafundisha wakazi wengine njia za kuwafukuza tembo wanapoingia mashambani. Hii itasaidia kuhakikisha uendelevu wa kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na changamoto za wanyamapori.
Pichani ni Askari wa Uhifadhi wa Kijiji (VGS)
Afisa Wanyamapori na Maliasili wa Wilaya ya Tunduru, Bw. Dunia Almas, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kupunguza migongano kati ya wanyamapori na binadamu. Amesema uzio wa pilipili umepunguza changamoto hii kwa asilimia 85.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Bw. Bosco Mwingira, anasema matukio ya uvamizi wa mashamba yanaongezeka hasa wakati mazao yanapokuwa yanakomaa, na kuvutia wanyama hao. Anaongeza kuwa Wilaya inatenga shilingi milioni 15 kila mwaka kununua vifaa vya kuwatisha na kuwafukuza tembo. Bw. Mwingira pia anataja kuwa ukusanyaji wa mapato ya wilaya umeongezeka kutoka shilingi bilioni 4.8 hadi bilioni 5.6, ambapo sehemu kubwa ya fedha hizo hutumika kutoa huduma za kijamii.
Pichani ni Bw. Bosco Mwingira ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
Imetolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,
Orpa Kijanda,
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.