Kamati ya Lishe ya Wilaya ya Tunduru imefanya kikao chake cha kawaida cha kila robo leo katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 na kuweka mikakati ya kuimarisha afua za lishe katika jamii.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ndugu Chiza Marando, na kuhudhuriwa na wataalamu kutoka idara mbalimbali zikiwemo Afya, Kilimo, Elimu, Maendeleo ya Jamii, pamoja na taasisi za maji na usafi wa mazingira kama RUWASA na TUUWASA.

Akifungua kikao hicho, Ndugu Marando alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa sekta zote katika kutekeleza shughuli za lishe kwa ufanisi, hasa katika shule, ili kupunguza changamoto za lishe duni kwa watoto.
“Tunataka kuona kila mwanafunzi anapata angalau mlo mmoja akiwa shuleni. Kamati ihakikishe inatembelea shule zenye changamoto za utoaji chakula ili kuhamasisha wazazi na jamii kuchangia chakula shuleni. Hatua hii itasaidia kuongeza ufaulu, hasa katika shule zenye matokeo duni,” alisema Ndugu Marando.
Katika kikao hicho, Kamati ilipokea taarifa ya hali ya lishe kwa kipindi husika, ambapo ilibainika kuwepo kwa changamoto kadhaa, ikiwemo upungufu wa maji safi na salama katika baadhi ya maeneo ya vijijini hali inayochangia magonjwa ya milipuko.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Wilaya ya Tunduru, Ndugu Martin Kigosi, alihimiza kuendelea kusimamia kilimo cha mazao ya lishe kama mahindi lishe na maharage lishe mashuleni, ili kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye virutubishi. Alibainisha kuwa utekelezaji wa kiashiria hicho bado uko chini na unahitaji kupewa kipaumbele zaidi.

Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.