Serikali ya Wilaya ya Tunduru imeendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, sambamba na kuimarisha hatua za kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya, Viongozi wa Dini, Wazee Maarufu, Mamwenye, Masultani na Machifu, Maafisa Tarafa, Wakuu wa Idara, pamoja na viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo viongozi wa Bodaboda, Bajaj, Guta, AMCOS, Chama cha Mpira wa Miguu, Wasafirishaji na Wachimba Madini.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Denis Masanja, ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa amani, utulivu na kuzingatia sheria za nchi.
“Uchaguzi wetu utafanyika kwa amani na utulivu. Vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kupiga kura katika mazingira salama. Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani,” alisema Mhe. Masanja.
Aidha, kikao hicho kimejadili kwa kina changamoto ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji, ambapo Mhe. Masanja alieleza kuwa serikali imeanza operesheni maalum ya kuwabaini na kuwaondoa wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa, kuvamia mashamba au kufanya uharibifu wa mazao ya wakulima.
“Kila kijiji kina Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi unaoainisha maeneo ya kilimo, makazi na malisho. Wafugaji wanaoingia kinyume na mipango hiyo wanavunja sheria. Tumewakamata baadhi yao na hatua za kisheria zinaendelea. Hatutasita kumfikisha mahakamani yeyote atakayekiuka taratibu hizi,” alisisitiza DC Masanja.
Mhe. Masanja pia aliwaonya wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi dhidi ya wafugaji wanaoingia kiholela katika maeneo yao, akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa Kamati za Maridhiano za Vijiji au kwa viongozi wa Serikali za Mitaa mara wanapobaini uwepo wa mifugo isiyoruhusiwa.
“Tunaendelea kufanya kazi bega kwa bega na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha migogoro hii inakomeshwa. Tunawaomba wananchi wafuate sheria na kutoa taarifa mapema badala ya kujihusisha na vitendo vya kujichukulia hatua wenyewe,” aliongeza.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.