Kikao cha robo ya kwanza cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya Kata na Wilaya kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kimefanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru kikiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Denis Masanja.

Kikao hicho kiliwakutanisha mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, wataalam wa afya na lishe, watendaji wa kata, wawakilishi wa sekta mbalimbali, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa mpango wa lishe katika robo ya kwanza na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za lishe kwenye jamii.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Denis Masanja aliwataka watendaji wa kata na wataalam kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo majukumu yao katika kusimamia mkataba wa lishe ili kupunguza changamoto za udumavu na utapiamlo kwa watoto na makundi mengine yaliyo katika hatari.
“Ni muhimu kila mmoja wetu kuwa na uwajibikaji wa dhati. Mikataba ya lishe si nyaraka tu, bali ni mwongozo wa kutuongoza namna ya kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na afya bora kupitia lishe sahihi,” alizungumza DC Masanja “Ajenda ya Lishe inatakiwa kuwasilishwa kwenye kila mkutano mkuu wa kijiji katika maeneo yetu”.
Katika kikao hicho, taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe kwa robo ya kwanza ziliwasilishwa na Afisa Lishe wa Wilaya ya Tunduru Ndg.Martin kigosi kujadiliwa kwa pamoja.

Wajumbe walikubaliana kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya lishe, kuboresha utendaji wa kamati za lishe ngazi ya kata na vijiji, na kuimarisha ushirikiano kati ya idara na sekta mbalimbali ili kuhakikisha malengo ya lishe ya wilaya hiyo yanafikiwa.
Kikao kiliisha kwa kuweka maazimio ya pamoja ambayo yatafanyiwa kazi katika robo inayofuata ili kuboresha zaidi huduma za lishe kwa wananchi wa Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.