Leo tarehe 24 Oktoba, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius S. Masanja, amefanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji uliopo katika Kijiji cha Msinji, Kata ya Ligoma, Tarafa ya Namasakata, Wilaya ya Tunduru.
Akiwa eneo la Mradi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tunduru, Mhandisi Maua Mgalla, alitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo ambapo alieleza kuwa Mradi huo una thamani ya Shilingi 1,069,000,000/= na hadi sasa umefikia asilimia 67 ya utekelezaji wake. Aliongeza kuwa Mradi huo unatarajiwa kukamilika mara baada ya Serikali kutoa fedha za kukamilisha sehemu iliyosalia, na utakapoanza kazi utatatua tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Kijiji cha Msinji.
Mkuu wa Wilaya aliupongeza uongozi wa RUWASA kwa usimamizi mzuri wa Mradi huo na akasisitiza umuhimu wa kuharakisha ukamilishaji wake ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya maji mapema. Aidha, alimtaka Meneja wa RUWASA kufuatilia kwa karibu malipo ya fedha zinazotakiwa kulipwa kwa Mkandarasi wa Mradi huo ili kazi zisikwame.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja alimuelekeza Meneja wa RUWASA kuangalia uwezekano wa kuchimba kisima cha dharura kijijini hapo, ambacho kitaanza kutoa huduma kwa wananchi wakati wakisubiri kukamilika kwa Mradi mkubwa wa maji unaoendelea kutekelezwa katika eneo hilo.
Mradi huo unatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Kijiji cha Msinji ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa muda mrefu.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.