Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imeungana na mataifa mengine duniani kwa kuzindua rasmi Wiki ya Unyonyeshaji Duniani. Uzinduzi huu umefanyika katika viwanja vya Baraza la Idd, ukiwa na lengo kuu la kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa afya bora ya watoto.

Mgeni rasmi katika hafla hii alikuwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Daktari Wilfred Rwechungula. Katika hotuba yake, Daktari Rwechungula alisisitiza umuhimu wa kuzingatia unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto wachanga kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza tangu kuzaliwa. Alieleza kuwa katika kipindi hicho, mtoto hahitaji kupewa maji, chakula mbadala, au vinywaji vingine, Alieleza kuwa kwa kufanya hivyo, mtoto anapata virutubisho vyote muhimu, kinga dhidi ya magonjwa, na uhusiano wa karibu na mama yake.
Daktari Rwechungula aliongeza kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama unasaidia kumlinda mtoto dhidi ya magonjwa mbalimbali, unachangia katika maendeleo ya ubongo wake, na pia huimarisha kifungo cha upendo kati ya mama na mtoto. Aliwahimiza kina mama kuepuka kumpatia mtoto maji, chai, au chakula kingine chochote mbadala katika kipindi hicho cha miezi sita, kwani kufanya hivyo kunaweza kudhoofisha kinga ya mtoto na kumsababishia matatizo ya kiafya. Aliongeza kuwa maziwa ya mama yana kila kitu anachohitaji mtoto kwa ukuaji wake mzuri na salama.
Wiki hii ya unyonyeshaj inatarajiwa kutumika kama jukwaa la kuongeza uelewa katika jamii kuhusu faida za unyonyeshaji, changamoto zinazowakabili akina mama wengi, na namna bora ya kuzishinda. Waliohudhuria uzinduzi huo walipata fursa ya kupata elimu na ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya kuhusu unyonyeshaji sahihi.

Wiki ya Unyonyeshaji Duniani, inayoangazia umuhimu wa maziwa ya mama kwa afya ya watoto, inaongozwa na kauli mbiu "Thamini unyonyeshaji: Weka mazingira wezeshi kwa mama na mtoto." Kauli mbiu hii inalenga kusisitiza kwamba unyonyeshaji sio jukumu la mama pekee, bali ni jukumu la jamii nzima. Inatoa wito kwa jamii, waajiri, na taasisi mbalimbali kuunda mazingira rafiki na yanayowezesha akina mama kunyonyesha watoto wao bila vikwazo. Kwa mfano, kuwepo kwa vyumba maalum vya kunyonyesha maofisini, muda wa kutosha wa likizo ya uzazi, na kuondoa unyanyapaa unaoweza kumfanya mama ajisikie vibaya kunyonyesha hadharani. Kwa kuthamini na kuweka mazingira wezeshi, tunahakikisha watoto wanapata lishe bora na kukuza kizazi chenye afya na nguvu.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.