UJENZI WA SOKO LA KIMATAIFA LA MADINI YA VITO WAENDELEA, TUNDURU
Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru inashirikiana na wadau wa maendeleo wilayani humo kukamilisha ujenzi wa soko jipya la kisasa la madini ya vito ambalo litakuwa soko kubwa zaidi Afrika Mashariki kwa madini ya vito.
Kwa mujibu wa Chiza Marando, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, ujenzi huo ulioanza mwishoni mwa Disemba 2023 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Aprili 2024, utagharimu Shilingi 1,087,000,000 (Bilioni 1.087) na jengo litakuwa na uwezo wa kutumiwa na kampuni 155 za madini ya vito kwa wakati mmoja.
Ndg. Chiza Marando ameweka bayana kuwa zaidi ya kampuni 130 zimeshaomba nafasi ya kufanyia biashara kwenye soko hilo na kwamba eneo la soko lina uwezo wa kubeba makampuni zaidi ya 500 ikiwa makampuni yataendelea kujitokeza.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Wakili Julius Mtatiro akiambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, ametembelea ujenzi huo na kupongeza sana hatua hiyo muhimu yenye tija kwa mustakabali wa rasilimali ambazo ziko Tanzania.
DC Mtatiro ameielekeza Halmashauri ya Tunduru kukamilisha haraka ujenzi huo na kuhakikisha soko linaanza kufanya kazi kwa wakati. Mtatiro amesema soko hili la pamoja likianza litapunguza vitendo vya utoroshaji wa madini ya vito wilayani humo, ambavyo vinafanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu na kupelekea serikali kukosa mapato na kodi.
Mtatiro amesisitiza kuwa soko hili likianza serikali haitaruhusu tena masoko madogo madogo kama Tudeco na Generation yaendelee na kazi kwani utitiri wa masoko hayo na kukosa soko la pamoja kumekuwa chanzo cha utoroshaji wa madini, biashara za madini ya vito nje ya masoko, biashara za madini ya vito majumbani, kukosa ushindani wa bei ya madini ya vito, serikali kukosa kodi na mapato na mengine madhara mengine mengi.
DC Mtatiro ameelekeza kampuni za madini ambazo zinafanyia kazi zake kwenye masoko madogo madogo ya madini wilayani humo zijiandae kuhamia kwenye Soko la Pamoja la Kimataifa la Madini ya Vito na kwamba kukiuka kuhamia kwenye soko hilo ni mbinu ya kuhujumu maelekezo ya serikali na maslahi ya nchi na kwamba serikali itachukua hatua.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, Afisa Migodi wa Wilaya ya Tunduru Ndg. Emmanuel Bushi ameeleza kuwa Soko Jipya la Pamoja la Kimataifa la Madini ya Vito ni mkombozi wa wachimbaji wadogo wadogo wa Madini ya vito wilayani humo na kwamba watapata ushindani na bei zenye tija kuliko hivyo sasa.
Afisa huyo ameishukuru sana Serikali kwa maono makubwa na kufafanua kuwa soko hilo jipya litafanya kazi ya usimamizi wa madini ya vito iwe nyepesi kwani hakutakuwa na mianya kama ilivyo sasa ambapo wilaya ina masoko madogo madogo.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.