Siku ya lishe na afya iliadhimishwa katika Shule ya Sekondari Tunduru, Wilayani Tunduru. Shughuli hiyo ilihudhuriwa na Afisa lishe, Afisa Ustawi wa Jamii, Mwalimu Mkuu, na wanafunzi wa shule ya Sekondari Tunduru.
Maadhimisho hayo yaliongozwa na Afisa Lishe wa Wilaya ya Tunduru, Bi. Martha Kibona, ambaye alitoa hotuba yake ya kuhamasisha wanafunzi na jamii kuhusu umuhimu wa kula vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji na maendeleo ya mwili na akili.
Afisa Lishe wa Wilaya ya Tunduru, Bi. Martha Kibona, alitoa Elimu kuhusu lishe bora kwa kijana aliye katika umri wa balehe. Alisema kuwa Lishe bora ni muhimu kwa ukuaji na maendeleo yao, aliwashauri walimu na walezi wa wanafunzi kuhakikisha kuwa watoto wanapata mlo kamili unaozingatia lishe bora.
"Lishe bora ni muhimu kwa Afya njema," alisema Bi. Martha. "Wakati wa ukuaji, mwili unahitaji virutubisho muhimu ili kukua na kuendeleza akili. Vyakula vyenye virutubisho muhimu ni pamoja na matunda,mboga mboga, nafaka, na protini."
Afisa Ustawi wa Jamii Bwn. Nelson Yohana aliwaelimisha wanafunzi kuhusu maswala ya ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuzuia ukatili wa kijinsia katika jamii. Aliwataka wanafunzi kuwa waangalifu dhidi ya ukatili wa kijinsia na.Pia aliwahimiza waweze kuripoti vitendo hivi vya ukatili ili kuepuka madhara yatokanayo na matendo hayo.
Mwalimu mkuu wa shule ya Sekondari Tunduru alitoa shukrani kwa wageni waalikwa na wanafunzi walio shiriki kikamilifu kwa kujifunza kwa bidii juu ya lishe bora na afya. Aidha, aliwashauri wanafunzi kusimamia vyema tabia na afya zao.
Hafla hii ya siku ya lishe na afya ilikuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi, kwani walipata elimu muhimu juu ya jinsi ya kudumisha afya bora kwa njia ya lishe bora na mazoezi. Pia walitambua haja ya kuelimishwa juu ya maswala ya ukatili wa kijinsia katika jamii. Hivyo, wanafunzi walionekana kuwa wamepata hamasa ya kuanza kuboresha lishe zao na kuwa na ubunifu wa kujipanga katika mazoezi kwa ajili ya afya bora.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.