Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Tunduru, Bw. George Alanus Njogolo, Azungumza na waandishi wa habari mapema leo ofisini kwake, Lengo ni kuwashirikisha waandishi wa habari mbinu mbalimbali ambazo ni muhimu katika kufikisha ujumbe ili kuwaeleimisha wananchi juu ya Mapambano dhidi ya rushwa kabla ya uchaguzi,katika kipindi chenyewe cha uchaguzi na hata baada ya kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza katika kikao hicho Bwn Njogolo amesisitiza kuwa rushwa ni adui wa maendeleo na inapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote, ametoa wito kwa waandishi wa habari kuwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano katika kupambana na vitendo vya rushwa. Amewataka wananchi kuripoti mara moja kwa TAKUKURU au vyombo vingine vya sheria wanapogundua vitendo vya rushwa. Amewahakikishia kuwa taarifa zao zitalindwa.
“Tunategemea ninyi ndio mnaowafikia wananchi kwa kiwango kikubwa na kwa wakati mmoja, kwahiyo kama mtashirikiana vyema pamoja na TAKUKURU katika kufikisha Elimu tutaifikia jamii kwa kiwango kikubwa sana” Alisema Bwn Njogolo “Kila mwananchi ana wajibu na haki ya kuchagua kiongozi amtakaye kwa ajili ya maendeleo, tutoe taarifa za vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi kwa wagombea, wananchi lakini hata kwa viongozi mbalimbali ambao tunashiriki katika zoezi zima la uchaguzi kwa mwaka huu”
Aidha, amezitaja sababu mbalimbali zinazopelekea kuwepo kwa rushwa au viashiria vyake kipindi cha uchaguzi,ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maadili kwa jamii, kutokuwepo kwa mifumo sahihi ya kudhibiti, kuwepo kwa fursa ya kukiuka kanuni bila kubainika, misukumo ya kupita bila kupingwa na pia uelewa mdogo kwa wananchi
Bwn Njogolo aliwasisitiza waandishi wa habari kutoa taarifa muhimu kwa wananchi ili wakati utakapofika waweze kujitokeza na kujiandisha kwa wingi ili kutimiza na kutumia haki yao ya kuchagua kiongozi bora, na pia wachague kiongozi ambaye hatotumia aina yoyote ya ushawishi kama fedha au vitu kuwarubuni ili wamchague, kufanya hivyo watajikuta wanachagua kiongozi ambaye hana manufaa kwa jamii husika, aliongeza kusema, kiongozi bora ni yule atakayepita kutokana na uwezo wake wa kazi ya kuhudumia wananchi kwa uadilifu.
Wananchi wanatakiwa kuwa tayari kutoa taarifa katika vyombo vya sheria, na pia wasiogope kutoa taarifa wanapohitajika kwasababu lengo ni kutaka kushirikiana ili kuweza kuzuia na kupambana na rushwa. Pia waonapo viashiria vyovyote vya rushwa kutendeka wanatakiwa kupiga simu mara moja kupitia namba 113, kupiga namba hii ni bure na sio lazima kutaja jina lako, njia nyingine ya kueleza lalamiko ni kufika ofisi ya TAKUKURU moja kwa moja, Taarifa zako zitalindwa.
Imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,
Orpa Kijanda.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.