Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Tawa) ikishirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Tunduru imetoa elimu kwa viongozi wa ngazi ya kata na vijiji ya namna bora ya kukabiliana na wanyama waaribifu katika wilaya ya Tunduru.
Mafunzo hayo yalitolewa katika Tarafa sita ambazo ni Nakapanya,Lukumbule, Nalasi, Matemanga, Nampungu na Namasakata pia yalihudhuriwa na maafisa kilimo kata ,viongozi wa vijiji na kata pamoja na afisa wanyamapori wilaya ya Tunduru.
Akizungumza katika kikao na viongozi hao wa kata na vijiji Bi.Ashura Hassan, afisa uhusiano kutoka Tawa amesema , kusudi la elimu hii kwa viongozi ni kuwawezesha utoaji huduma ya uharaka kwa wananchi pasipo kutokea kwa athari kubwa unapotokea mgongano baina ya wanyama wakali na waharibifu katika maeneo yao.
"Tumeleta mafunzo haya kwenu, ikiwa ni njia bora ya kuwafikia wananchi kwa urahisi pamoja na kuwajengea uelewa mkubwa, ili kuwawezesha kukabiliana na wanyama hawa bila kuleta athari kubwa katika jamii." Alisema.
Aidha kwa upande wake Afisa Wanyamapori (W) Ndg. Dunia Almasi alielekeza mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu hasa Tembo, pia alitoa tahadhari na kuwasihi viongozi kufuata utaratibu na kutumia mbinu hizo kwa usahihi.
Wilaya ya Tunduru imepakana na hifadhi ya Wanyama ya Mwalimu Nyerere iliyokuwa ikijulikana kama Selous hapo awali, Tawa wakishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na wadau mbalimbali imejipanga kupunguza kwa kiasi kikubwa migongano ya Wanyamapori na Wanadamu.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.