Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya Tunduru Juma Zuberi Homera alipokuwa akikabidhi baiskeli (wheel Chair) kwa mwanafunzi mlemavu wa viungo, pamoja na mifuko kumi ya saruji ya kukarabati vyoo katika shule ya msingi Mchangani iliyopo wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma mapema leo.
Akizungumza na wananchi pamoja na vyombo vya Habari Afisa Elimu, Elimu Maalum mwalimu Albert Nakamata alitoa changamoto ya upungufu wa miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, na pia alisema kuwa jamii kuwaficha watoto hao hivyo kupelekea wilaya kukosa takwimu sahihi za idadi ya walemavu.
Mwalimu Albert aliendelea kusema katika shule ya msingi Mchangani kuna jumla ya wanafunzi wenye ulemavu wapatao 8 ikiwa wenye mtindio wa ubongo wanne na walemavu wa viungo wanne, kati yao saba ni wavulana na mmoja ni msichana.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Zuberi Homera akikabidhi mifuko kumi ya saruji kwa ajili ya ukarabati wa vyoo katika shule ya msingi Mchangani, katika picha aliyemshika mkono mkuu wa wilaya ni Mkurugenzi wa kampuni ya DNG ltd, mkuu wa shule ya msingi Mchangani aliyefunga ushungi pamoja na Diwani wa kata ya mchanga Mh. Abdalah Hairu
Alisema mwalimu Albert "tunaomba serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo tushirikiane katika kujenga shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwarahisishia katika upatikanaji wa elimu na pia kutoa changamoto kwa jamii kuwapeleka watoto hao shule na kuacha kuwaficha"
Akizungumza na wananchi wa kata ya mchangani, wanafunzi na vyombo vya Habari Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Zuberi Homera Kabla ya kukabidhi kiti cha magurudumu manne (wheel chair) kwa mwanafunzi mlemavu wa viungo Shaibu Halifa Mpoto alisema kwa mwaka wa 2017/2018 halmashauri kupitia mfuko wa Elimu Tunduru imetenga shilingi milioni 7,200,000 kwa ajili ya kununua mahitaji ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mkurugenzi wa Kampuni ya DNG ltd Ndg Geofrey Kalamba wanaojishughulisha na ununuzi wa Korosho akimkabidhi mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Homera Baiskeli kwa ajili ya mwanafunzi mlemavu wa viungo Shaibu Halifa Mpoto mapema leo katika shule ya Msingi Mchangani.
Juma Homera alisema fedha iliyotengwa itatumika katika kununua Wheel Chair nyingine tano kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, mafuta, kofia na miwani ya jua kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi ili kuwaweza kuishi katika mazingira tulivu wakati wa masomo yao.
Aliendelea kwa kuipongeza kampuni ya DNG LTDs ambao wamenunua baiskeli kwa ajili ya mwanafunzi Shaibu Halifa Mpoto, pia kuona jitihada za serikali katika kuboresha huduma za jamii na kuchangia takribani mifuko 150 ya saruji ambayo imeelekezwa katika miradi ya ujenzi katika shule, zahanati na kituo cha forodha Lukumbule.
Bi pauline Sosthenes Mdimu akiongea na wanafunzi wa shule ya msingi Mchangani kuwasisitiza umuhimu wa Elimu na kutilia mkazo katika Elimu kwani ndio ukombozi wa mwanadamu, ukishakombolewa kifikra mengine yote yanakuja.
Akitolea maelezo juu ya ukosefu wa miundombinu ya shule kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, mkuu wa wilaya ya Tunduru alisema serikali ina mpango mkakati wa kuanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Extended ili kutoa fursa ya elimu kwa kundi hili ambalo linakumbana na changamoto za kukosa haki ya kupata elimu.
"Tuna mpango wa kujenga shule ya mahitaji maalum ya wilaya ambayo itakuwa na uwezo wa kusajili wanafunzi kuanzia darasa la awali hadi sekondari, watakuwa wanakaa shuleni ili kuweza kuhudumiwa vizuri kwani kuendelea kuwaacha katika shule Jumuishi hawawezi kusoma kama wanafunzi wa kawaida hasa kwa kuwalenga wale wenye mtindio wa ubongo, bubu viziwi na walemavu wa akili" Juma Homera alisema
baadhi ya viongozi walioshiriki katika zoezi la kukabidhi baiskeli kwa mwanafunzi mwenye ulemavu wa viungo pamoja na Mifuko kumi ya saruji katika shule ya Msingi Mchangani.
Pia alisema mwanafunzi Shaibu Halifa Mpoto amekuwa akibebwa mgongoni na bibi yake kufika shuleni na kurudi na wakati mwingine rafiki zake ndiyo humbeba, ambaye amekuwa katika hali hiyo toka akiwa darasa la nne hadi sasa yupo darasa la saba.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru akifanya maribio ya Baiskeli (wheel chair) baada ya kumkabidhi mwanafunzi shaibu Halifa aliyekaa katika baiskeli hiyo.
"Hali hii ndio iliwagusa wamiliki wa Kampuni ya DNG waliokuwa wananunua zao la korosho wilayani Tunduru kuona ni vyema basi wakatoa mchango wa baiskeli kwa mwanafunzi huyu ili iweze kumsaidia na kumpunuzia mzigo bibi yake aliyekuwa anambeba mgongoni kila siku kumpleka shuleni na kumrudisha nyumbani" alisema Mkuu wa Wilaya.
Naye bibi wa mtoto Shaibu Halifa Mpoto, Bi Fatu Kauma Omari alisema kuwa anaishukuru serikali pamoja na wadau wa maendeleo waliowasaidia kumpatia mjukuu wake baiskeli, pia wanafunzi kwa kutomtenga mjuu wake, pia aliwapongeza walimu wa shule ya Msingi Mchangani kwa jitihada na moyo wa upendo wanaouonesha kwa mjuu wake.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.