Naibu Katibu Mkuu, Elimu (OR TAMISEMI) Dkt. Charles Msonde, amefanya mkutano na walimu wa wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma. Mkutano huo ulihudhuriwa na walimu kutoka shule zote za msingi na sekondari za wilaya ya Tunduru.
Akizungumza katika mkutano wa walimu wa wilaya hiyo uliofanyika tarehe 21 Novemba 2023, Mwl. Nkwama alisema kuwa uadilifu ni nguzo muhimu katika utendaji kazi wa walimu, na kwamba walimu wanapaswa kuwa waadilifu katika kila jambo wanalofanya, ikiwa ni pamoja na kufundisha, kutathmini wanafunzi, na kusimamia taarifa za wanafunzi.
“Walimu wangu mnafanya kazi kubwa sana, tembeeni kifua mbele, msijipe presha katika utendaji kazi wenu, mnastahili pongezi za dhati” alisema Dkt. Msonde “Mwalimu ndio msingi wa fani na ujuzi wowote duniani, tunafanya kazi ya kulea watoto kwa kuzingatia misingi na maadili ya kitanzania, jukumu hili tuliachiwa na baba wa taifa, hayati Mwal. J.K. Nyerere”
Dkt. Msonde pia aliwasisitiza walimu wa wilaya ya Tunduru kujipanga kwa ajili ya mtaala mpya wa elimu utakaoanza kutumika kwa mwaka wa masomo 2024/2025. Alisema kuwa mtaala huo unalenga kuboresha ubora wa elimu nchini, na kwamba walimu wanapaswa kujifunza kuhusu mtaala huo ili waweze kuutekeleza kwa ufanisi.
Aidha, Dkt. Msonde alitoa ahadi ya kuhakikisha madeni yote ya walimu wa wilaya ya Tunduru yanalipwa, ikiwa ni pamoja na madeni ya uhamisho na likizo. Alitoa agizo kwa idara ya Elimu wilaya kuhakikisha kuwa madeni hayo yatalipwa haraka iwezekanavyo. Alisema kuwa Serikali inatambua mchango wa walimu katika maendeleo ya elimu nchini, hivyo inawajibika kuhakikisha kuwa wanalipwa stahiki zao kwa wakati.
Akihitimisha mazungumzo na walimu Dkt. Msonde, alilisisitiza juu ya wanafunzi wote waliohitimu darasa la saba kujiunga na masomo ya pre-form one ili waweze kupata maandalizi bora kabla ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza. Ameongeza kuwa serikali ina nia ya kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapata elimu bora, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanawapeleka watoto wao shule.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.