Msimu wa Ukusanyaji wa Ufuta kwa ajili ya mauzo ya zao la ufuta katika Wilaya ya Tunduru umefunguliwa rasmi leo Mei 22, 2024.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mheshimiwa Simon K. Chacha wakati wa Mkutano wa wadau wa zao la ufuta uliofanyika wilayani humo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani, viongozi wa Vyama vya Msingi, mameneja na makarani wapimaji.
Mheshimiwa Chacha amesisitiza viongozi wa AMCOS na makarani kusimamia ukusanyaji wa ufuta kwa uadilifu ili kuleta tija kwa wakulima wa zao hilo.
“tunapokwenda kusimamia Ukusanyaji wa zao hili , tunatakiwa kuwa na vitu vitatu, ambavyo ni Uadilifu, Uaminifu na Ushirikiano baina yetu”. Alisema DC Chacha.
Mhe, Chacha ameongeza kuwa minada ya ufuta wilayani Tunduru itaanza Mei 30, 2024 na itafanyika kidijitali kupitia mfumo wa Soko la Bidhaa (TMX) kwa kushirikiana na Chama Kikuu cha Ushirika wa Masoko ya Mazao Tunduru (TAMCU LTD), ambapo mnada wa kwanza utafanyika katika Tarafa ya Nalasi, Kijiji cha Molandi.
Mwenyekiti wa TAMCU LTD, Ndg. Mussa A. Manjaule, amewasisitiza makarani na mameneja kushirikiana na Bodi ya Uongozi wa Vyama ili kuhakikisha usimamizi bora wa zoezi la ukusanyaji wa ufuta kwa msimu wa 2024/2025.
Meneja Mkuu wa TAMCU LTD Ndg, Marcelino Mrope amesema amehakikisha kuwa TAMCU LTD inatoa vifaa muhimu vitavyowezesha zoezi la ukusanyaji katika maghala ya kukusanyia ufuta, vikiwemo vifungashio, mizani, vipima unyevu, usafiri, na ghala za kuhifadhia mazao.
Aidha, Mrope ameendelea kuelezea kuwa uzalishaji wa zao la ufuta umeongezeka kwa asilimia 53.09% kutoka msimu wa 2022/2023 hadi msimu wa 2023/2024, ukifikia kgs 4,800,997.20 kutoka kgs 2,548,815. Bei ya zao la ufuta pia imeimarika kwa msimu wa 2023/2024, kwa wastani wa Tshs. 3,684.54 ikilinganishwa na Tshs. 3,019.80 kwa msimu wa 2022/2023.
Msimu huu unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wakulima wa zao la ufuta wilayani Tunduru kutokana na ongezeko la uzalishaji na bei bora ya soko.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.