Mradi wa Stawisha Maisha unatarajiwa kuanzishwa hivi karibuni katika Wilaya ya Tunduru, ukiwa na lengo la kuwanufaisha akina mama wajawazito na wenye watoto chini ya miaka mitano (0-5). Mradi huu unalenga kuelimisha jamii kuhusu masuala ya lishe bora, hasa kwa watoto wadogo, katika mkoa wa Ruvuma unaojulikana kuwa na viwango vya juu vya udumavu licha ya kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula.
Serikali kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto na wanawake katika mataifa yanayoendelea (UNICEF), imeweka mikakati ya kupambana na udumavu katika mkoa wa Ruvuma, Mradi wa Stawisha Maisha ni sehemu ya mikakati hii. Wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa wilaya tatu zilizochaguliwa kushiriki katika mradi huu wa majaribio, wilaya nyingine ni pamoja na Wilaya ya Mbogwe-Geita, na Wilaya ya Kongwa iliyopo Mkoani Dodoma.
Akitolea ufafanuzi wa Mradi huu, Afisa ufuatiliaji wa Wilaya ya Tunduru kutoka makao makuu ya TASAF ambayo yapo Dar es salaam, Bw. Lazaro Mapimo alisema Mkoa wa Ruvuma, licha ya kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha mazao ya chakula kwa wingi, lakini una kiwango kikubwa cha hali ya udumavu. Hii inamaanisha kuwa watoto wengi hawapati virutubisho stahiki na vya kutosha kwa ukuaji na maendeleo bora.
“Mradi wa Stawisha Maisha unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya kwa afya na ustawi wa mama na watoto katika Wilaya ya Tunduru. Kupitia elimu bora ya lishe, tunatarajia kupunguza viwango vya hali ya udumavu na kuboresha maisha ya jamii kwa ujumla” Alisema Bwn. Mapimo.
Mradi huu unapitia hatua za awali za kuunda vikundi vya walengwa. Pamoja na mafunzo mbalimbali watayopatiwa, wanachama wa vikundi hivi watapokea redio bure watakazotumia kusikiliza vipindi mbalimbali vya kuelimisha kuhusu lishe bora kwa mama na watoto.
Wananchi wa Wilaya ya Tunduru wanapewa wito kushirikiiana katika mradi huu kwa kuhamasisha akina mama wajawazito na wenye watoto chini ya miaka mitano kushiriki kikamilifu katika vikundi vitakavyoundwa na kusikiliza vipindi vya elimu ya lishe. Pamoja, tunaweza kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata lishe bora kwa ukuaji na maendeleo yao bora.
Imetolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,
Orpa Kijanda,
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.