Chama Kikuu cha Ushirika wa Masoko ya Mazao Tunduru (TAMCU LTD) kimefanya uzinduzi wa Mnada wa kwanza wa Ufuta uliofanyika Kijiji cha Molandi, Kata ya Marumba, Wilaya ya Tunduru Juni 04, 2024.
Mnada huo ulifanyika chini ya uongozi wa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Simon K. Chacha, na ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya.
Mnada huu umetumia Mfumo wa Soko la Bidhaa (TMX) kuendesha mnada kwa njia ya kidijitali. Mfumo huu mpya uliwezesha wanunuzi wanne kununua Ufuta wote Tani 701 zilizokuwa sokoni kwa uwazi na ufanisi.
Wakulima walifurahia sana kupata bei nzuri kwa mazao yao, kwani bei ya juu ilifikia 3,783 kwa kilo, bei ya chini 3,705 kwa kilo, na bei wastani 3,744 kwa kilo. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba wakulima wote walifanikiwa kuuza mazao yao yote katika mnada huo.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru aliwapongeza wakulima kwa mafanikio yao na kuwasisitiza kuendelea kuzingatia ubora na usafi wa zao la Ufuta ili liweze kushindana vyema katika soko la kimataifa. Aliwahimiza pia wazazi kutumia fedha wanazopata kutokana na mauzo ya mazao yao kuwekeza katika elimu ya watoto wao.
Mwenyekiti wa TAMCU LTD, Ndg. Mussa A. Manjaule, aliwahimiza wakulima wa Wilaya ya Tunduru kulima mazao mchanganyiko ili kuongeza tija na kipato chao. Aliamini kuwa mbinu hii itaboresha maisha ya wakulima na kukuza uchumi wa Wilaya ya Tunduru kwa ujumla.
Meneja Mkuu wa TAMCU LTD, Ndg, Marcelino Mrope, Ametoa pongezi kwa Wakulima wa Ufuta kwa kukubali kuuza ufuta wao, aidha, amewataka wakulima kuhakikisha akaunti zao za benki, ili kupelekea ufanisi katika ulipaji wa fedha zao.
Mnada wa Kwanza wa Ufuta umeonekana kuwa na mafanikio makubwa kwa TAMCU LTD, wakulima, na Wilaya ya Tunduru kwa ujumla. Mfumo mpya wa kidijitali umeonyesha uwezo wake wa kuboresha ufanisi wa minada, na wakulima wamepata faida nzuri kutokana na mauzo ya mazao yao.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.