Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza C. Marando ametoa maelekezo kuwa ujenzi ufanyike kwa masaa 24 ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kabla ya tarehe 30/09/2023.
Agizo hili amelitoa tarehe 11/09/2023 Katika ziara ya kikazi ya kukagua na kutembelea miradi ya maendeleo katika kata ya Nakapanya, Tuwemacho, Tinginya na Ligoma zilizopo Wilayani Tunduru. Mkurugenzi Mtendaji amesisitiza umuhimu wa kamati ya ujenzi pamoja na wataalamu kushirikiana ipasavyo na kuwasimamia wajenzi ili kazi ifanyike kwa ufanisi na kumalizika kwa wakati uliopangwa. Ushirikiano na usimamizi wa karibu utahakikisha kuwa miradi ya maendeleo inakidhi viwango na inakamilika kwa wakati uliopangwa.
“kuwepo na ushirikiano mzuri baina ya wataalamu, kamati ya ujenzi na wajenzi ni muhimu sana ili ujenzi ukamilike vizuri. Ni muhimu sana timu hii iwe tayari kutafuta suluhisho la haraka pale ambapo tatizo linatokea ili kupunguza madhara yanayoweza tokea, nitahakikisha umeme unakuwepo muda wote ili ujenzi uendelee kufanyika kwa masaa yote 24”. Mkurugenzi Mtendaji alisisitiza.
Kukamilisha miradi ya maendeleo ni jambo muhimu sana kwani huathiri moja kwa moja maisha ya wananchi. Kupitia ukaguzi wa mara kwa mara, wilaya ya Tunduru itakuwa na uhakika kwamba mradi unatekelezeka vizuri bila matatizo yoyote. Wananchi watakuwa na imani zaidi kwamba Serikali yao inafanya juhudi za dhati za kukidhi mahitaji yao.
Hata hivyo, ukaguzi wa miradi ya maendeleo ni hatua muhimu sana katika kudhibiti utekelezaji wa miradi hiyo. Kwa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji ameonesha nia ya kufuatilia maendeleo ya miradi na kuhakikisha kuwa hakuna ucheleweshaji au upungufu wowote. Hatua hii itasaidia kuimarisha ufanisi katika utekelezaji wa miradi huku ikiruhusu wilaya ya Tunduru kukamilisha miradi yake ya maendeleo kwa wakati uliopangwa.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda,Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.