Tunduru 19/12/2019
Halmashauri inatarajia kujenga vyumba Zaidi ya 30 vya madarasa katika shule za sekondari na msingi ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya kupokea wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 pamoja na kupunguza msongamano katika shule za msingi wilayani Tunduru.
Akiwasilisha bajeti ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa katika kikao cha kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango Ndg. Jumanne Mwankhoo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg Gasper Z. Balyomi amesema upungufu huu umesababishwa na ongozeko kubwa la ufaulu wa wanafunzi katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba kwa mwaka 2019.
Aliendelea kufafanua kuwa jumla ya wanafunzi 4959 waliofanya mtihani wa darasa la saba wamefaulu na kupangiwa shule hivyo kuwa na upungufu wa vyumba Zaidi ya 80 katika shule za sekondari wilayani Tunduru.
“wanafuzni 4959 wamepangwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 lakini miongoni mwa hao ni wanafunzi 1520 pekee ndio waliopata vyumba vya madarasa na zaidi ya wanafunzi 3439 hawatakuwa na madarasa hivyo kufanya kuwa na upungufu wa Zaidi ya vyumba 86” alisema Afisa Mipango.
Mwankhoo amesema fedha hizi zitatumika katika ujenzi wa vyumba 33 vya madarasa kwa elimu sekondari na msingi, ukamilishaji wa daharia katika shule mbili za sekondari za Nakapanya na Masonya na ujenzi wa matundu 66 ya vyoo katika shule za msingi 11 za Likweso, Chikomo, Misufini, Chiwana, Msinji, Machemba, Chajila, Mkandu, Nasya, Ipanji na Mbati ya leo.
Aidha fedha hizo zimetokana na makusanyo ya mfuko wa maendeleo wa wilaya ya Tunduru ulioanzishwa kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali lakini kipaumbele kikiwekwa katika kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na samani zake katika shule za sekondari na msingi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.