Na Theresia Mallya -Tunduru
Katika utekelezaji wa sera ya michezo ya serikali ya awamu ya tano ya kuhamasisha kusimamia michezo katika ngazi zote hapa nchini kwa kuendeleza matamasha ya michezo kuanzia ngazi za vijiji,kata, wilaya, mkoa hadi taifa, uzinduzi wa ligi ya DC Homera Cup imezinduliwa na mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe.Juma Zuberi Homera mwishoni mwa juma.
Akizungumza katika uzinduzi wa ligi ya DC Homera Cup uliofanyika katika viwanja vya kijiji cha Nangunguru Kata ya Nandembo mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe.Juma Zuberi Homera alisema mashindano haya ni kwa ajili ya kupata timu 16 zitakazowakilisha tarafa katika michezo ngazi ya wilaya.
wachezaji wa timu ya super wakiwa katika maandalizi ya ufunguzi wa mechi kati yao na timu ya chimbuko kutoka katika kijiji cha majala katika Mechi ya ufunguzi wa ligi ya DC Homera Cup inayotimua vumbi katika viwanja mbalimbali wilayani Tunduru.
“Mashindano haya yanalenga kupata timu mbili kutoka kila tarafa zitakazowakilisha tarafa kwenye mashindano ngazi ya wilaya na baadaye kupata timu moja ya wilaya” alisema mkuu wa wilaya ya Tunduru.
Mkuu wa wilaya aliahidi zawadi zifuatazo kutolewa kwa washindi ngazi ya tarafa ikiwa ni pamoja na mshindi wa kwanza kupewa zawadi ya jezi,mpira na fedha tsh 150,000, mshindi wa pili fedha taslimu laki moja, jezi, na mpira ana mshindi wa tatu kupata jezi na fedha shilingi sitini elfu (50,000).
Akitaja zawadi nyingine zitatolewa kwa timu yenye nidhamu, mfungaji bora na mwamuzi aliyechezasha mechi kwa kuzingatia kanuni 17 za fifa.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe.Juma Zuberi Homera akifuatilia mechi ya Ufunguzi wa Ligi ya DC Homera Cup iliyopigwa na timu ya chimbuko kutoka kijiji cha majala na super ego ya kijiji cha Nangunguru iliyopigwa katika kiwanja cha Kijiji cha Nangunguru ambapo hadi mchezo unaisha walitoshana nguvu ya Goli 1-1.
Kwa upande wa wachezaji na walimu wao walipongeza kuanzishwa kwa ligi ya DC Homera Cup kwani inaongeza hamasa kwa wananchi na kutoa fursa kwa vijana kuonesha vipaji vyao, kujenga umoja na ushirikiano kati ya kijiji na kijiji, kata na hata tarafa, na kufahamiana,zaidi fursa ya kusongambele zaidi katika kufikia ndoto walizojiwekea.
“Tunaomba michezo hii iwe endelevu angalau ifanyike mara mbili au tau kwa mwaka kwa ajili ya kuwajenga vijana wetu, na wadau wengine wajitokeze katika kusapoti michezo katika wilaya yetu” alisema mwalimu wa timu ya Chimbuko ya kijiji cha Majala.
Naye mwalimu wa timu ya Sevenup kutoka Kata ya Namakambale Bw. Mkakia aliomba usimamizi wa chama cha michezo wilaya kuwa wabunifu ili kuendeleza michezo ndani ya wilaya na kuwaunganisha wakazi wa Tunduru kwani wapo vijana wengi wenye vipaji lakini hawapati nafasi ya kujiendeleza.
Tunampongeza sana Mkuu wetu wa Wilaya kuanzisha ligi hii kwani inatoa hamasa kwa vijana wengi na wananchi wanapenda michezo sana, niwaombe vingozi wa chama cha michezo wilayani Tunduru muendeleze michezo na kuwa wabunifu ili tutengeneze timu zitakazotufikisha mbali zaidi ya hapa tulipo sasa” alisema Mkaki mwalimu wa timu ya Sevenup Namakambale.
Hata hivyo ligi hii ya DC Homera Cup inatimua vumbi katika viwanja mbalimbali katika tarafa zote saba (7) za Mlingoti, Nampungu, Matemanga, Nakapanya, Namasakata, Nalasi na Lukumbule kwa lengo la kuhamasisha lakini pia kuibua vipaji kwa vijana wengi na kutoa fursa ya ajira.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.