Na Theresia Mallya- Tunduru
15/05/2019
Akiwa katika mkutano wa hadhara kijiji cha Azimio mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe.Juma Zuberi Homera aliwaagiza maafisa tarafa wa tarafa za Lukumbule na Nampungu kusimamia na kutatua mgogoro wa mipaka uliopo katika kijiji cha Machemba na Azimio.
Maagizo hayo yamekuja baada ya wananchi wa kijiji hicho kulalamika mbele ya mkuu wa wilaya juu yakuchukuliwa eneo lao na wananchi wa kijiji cha Machemba kwa muda mrefu huku ramani ya mipaka ikiwa ni tofauti na ile iliyotolewa na Idara ya Ardhi na Maliasili ya Halmashauri ya Tunduru.
Akitoa maelezo ya mgogoro huo wa mipaka katika kijiji hicho Ofisa Mtendaji wa kata ya Mtina Bi.Judith Mwamili alisema kuwa tatizo hilo limefanyiwa kazi na afisa ardhi na maliasili kwa kusoma ramani ya mipaka kwa kutumia GPS ili kutambua mipaka kuanzia mwaka 2016.
Alisema baada ya vipimo kufanyika eneo lenye mgogoro lilionekana kuwa ndani ya kijiji cha machemba lakini uongozi wa kijiji cha Azimio walikataa ramani na kudai kuwa wanataka kutumia ramani ya mwaka 1979 badala ya ramani iliyoletwa na idara ya ardhi ya mwaka 2008.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe.Juma Zuberi Homera akiongea na wananchi wa Kijiji cha Azimio ambao hawapo kwenye picha katika mkutano wa hadhara wa kuslikiliza na kutatua kero na changamoto za wananchi.
Naye mkuu wa wilaya ya Tunduru akaagiza vijiji vyote viwili yaani Machemba na Azimio kuunda kamati ya maridhiano itakayoshirikiana na maafisa tarafa na watumishi wa Idara ya Ardhi na Maliasili ndani ya mwezi mmoja ili kusuluisha mgogoro uliopo.
Aidha kwa upande wa kilimo katika skimu ya umwagiliaji ya madaba kwa baadhi ya mabanio kutokufanya kazi toka mradi kukabidhiwa kwa halmashauri mkuu wa wilaya Juma Homera alisema serikali inafanyia kazi kwa kushirikiana na wizara ya kilimo, ushirika na umwagiliaji kutatua changamoto iliyopo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kumekuwa na changamoto nyingi kwani mradi huo ulijengwa chini ya kiwango na sio huo tuu ila ni miradi yote katika skimu za Madaba, Kitanda, Misyaje na Lelolelo ilitekelezwa chini ya kiwango.
wananchi wa kijiji cha Azimio wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera ambaye hayuko katika picha.
Serikali kwa kuliona hilo ili kuwasaidia wananchi marekebisho yatafanyika kupitia mradi wa ASDP II(Agricultural Sector Development Program) ili kuondoa changamoto kwa wananchi na kuokoa fedha zilizotumiwa na serikali katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji wilayani Tunduru na Tanzania kwa ujumla.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.