Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru imeungana na watumishi pamoja na wananchi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya wilaya kama sehemu ya shughuli za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Akizungumza baada ya kumaliza kufanya usafi katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru, Ndg. Milongo Sanga, amesema zoezi hili la usafi liwe endelevu katika kudumisha hali ya usafi katika Wilaya ya Tunduru.
“Niwashukuru kwa kujitokeza katika zoezi hili la kufanya usafi, tulifanye kama jadi yetu ili kudumisha usafi katika mazingira yetu”. Alisema Sanga.
Aliongeza kuwa, katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, tarehe 25 Aprili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dr. Samia Suluhu Hassan, atahutubia taifa kuelekea miaka 60 ya Muungano Tanzania,ambapo Wilaya ya Tunduru itashuhudia hotuba hiyo mubashara katika Viwanja vya Baraza la Idd kuanzia saa 3 kamili usiku. ambapo, kutakuwa na maonyesho ya wazi ya Televisheni kwa wananchi wote.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Ndg. Masanja Kengese, amewashukuru wananchi na watumishi kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hili la usafi. Amewataka wananchi kuendeleza zoezi hili la usafi katika maisha yao ya kila siku ili kudumisha mazingira safi na salama.
Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania yanaadhimishwa nchini kote kwa shughuli mbalimbali ikiwemo , Sala za kuliombea taifa, semina, na mashindano ya michezo. Maadhimisho haya yana lengo la kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania, pamoja na kukumbuka historia ya mapambano ya kupigania uhuru na umoja wa nchi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.