Zao la muhogo ni zao la tatu kwa umaarufu na umuhimu wilayani Tunduru likitanguliwa na mazao ya korosho na mpunga. Mapema jana katika ukumbi wa skyway hapa wilayani Tunduru kulikua na warsha ya kilimo cha muhogo kwa kutumia mbegu za kisasa. Warsha hiyo iliandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya International Institute of Tropical Agriculture (IITA). Baadhi ya viongozi walioshiriki katika warsha hiyo ni wawezeshaji kutoka IITA, MEEDA, Wizara ya Kilimo Taasisi ya Utafiti Kibaha, Madiwani, viongozi wa ngazi ya Halmashauri na wakulima wa mihogo wilayani Tunduru.
Akifungua warsha hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ndg Jonathan A Haule alisema “Ili kukabiliana na baa la njaa, mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na hali ya wananchi wengi kutegemea mazao ya korosho na mpunga ni wakati sasa wa kubadilika na kuona umuhimu wa kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa muhogo kwa kutumia mbegu bora za kisasa” Aliendelea kwa kutaja faida za kilimo cha muhogo kuwa ni zao linalotumika kwa chakula cha ugali, malighafi viwandani, kutengeneza maandazi, chapati, chipsi na ni zao linalostahimili ukame.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru ndugu Jonathan Haule (aliyesimama) akifungua warsha ya kilimo cha muhogo, kushoto kwake ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wiliya mh. Mbwana Mkwanda Sudi na anayefuta ni Makamu mwenyekiti wa Halmashauri mh. Mfaume Wadali.
Wawezeshaji hao kwa nyakati tofauti tofauti walieleza namna ya upatikanaji wa mbegu bora za zao la muhogo, uandaaji wa mashamba, huduma, uvunaji na soko la zao hilo.
Akizungumzia changamoto mwezeshaji kutoka IITA ndg Davis Mwakanyamale alibainisha baadhi ya magonjwa sugu yanayoshambulia zao hilo kuwa ni batobato na michirizi kahawia, na alitoa ushauri kwa wajumbe wa warsha hiyo kutumia mbegu bora za mihogo kama Mkuranga 1, Kipusa, Chereko na Kizimbani ambazo zina uwezo mkubwa wa kuvumilia ukame pia kupambana na magonjwa na mabadiliko ya tabia ya nchi, uwezo wa kuzaa sana zaidi ya tani 20 kwa hekta pia ni mbegu zinazokomaa mapema.
Timu ya wawezeshaji wa warsha ya kilimo cha muhogo, kutoka kushoto ni Bi. Hellen Kiozya (wizara ya kilimo taasisi ya utafiti Kibaha) Bw.Davis mwakatumbula (IITA),
Bw.Lokola Ndibalema (IITA) na Bw. Erick Muhongole kutokea taasisi ya MEEDA
Nao madiwani walitoa mapendekezo ya baadhi ya mbinu za kuongeza uzalishaji wa zao hilo kuwa ni kutafuta soko la uhakika, kutoa elimu ya uzalishaji kwa wananchi kupitia maafisa ugani wa Kata na wananchi kuwezeshwa upatikanaji wa mbegu bora za kisasa kwa bei nafuu.
Aidha kwa umoja wao madiwani hao walikubaliana na umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa zao hilo muhimu kwa chakula na biashara na kwamba kila mmoja ataenda kushawishi na kutoa Elimu kwa wananchi wake kuzalisha mbegu za mihogo bora kupitia vikundi vya wajasiliamali kwenye kata zao ili kuwa na mashamba ya mfano.
Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Tunduru Mh. Mbwana Mkwanda Sudi alihitimisha warsha hiyo kwa kuwashukuru wawezeshaji, viongozi na wadau kwa kusema “Halmashauri ina shauku ya kutimiza agizo la kuwa na viwanda vikubwa na vidogo vidogo vya uzalishaji na usindikaji, na ili kutimiza adhma hii Halmashauri yetu itatilia mkazo katika fursa hii kwa wakazi wa Wilayani Tunduru kuzalisha na kuanzisha viwanda vya usindikaji wa muhogo kwa matumizi ya chakula na viwandani”.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Mh. Mbwana Mkwanda Sudi akihitimisha warsha ya kilimo cha muhogo wilayani Tunduru.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria katika warsha ya kilimo cha muhogo wilayani Tunduru tarehe 09.03.2018
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.