Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, imefanya kikao cha kujadili utekelezaji wa masuala ya Lishe kutoka idara mbalimbali na vitengo, kwa kipindi cha robo ya nne (April – Juni 2023), katika ukumbi wa Halmashauri Agosti 8, 2023.
Kikao hiki kilikuwa na nia ya kuhakikisha kuwa mipango na Sera za Afya na Lishe zinatekelezwa kikamilifu ili kuboresha hali ya Lishe kwa Umma. Sera na mipango iliyofanikiwa mpaka sasa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa chakula bora na lishe bora kwa kila mtu, utoaji wa Elimu juu ya afya na lishe bora, kuweka sera na sheria zinazosaidia kuboresha lishe, kuendeleza kilimo cha mazao bora kama vile viazi Lishe, kilimo cha Matunda na mboga mboga, kuongeza upatikanaji wa Maji safi na salama, kutoa matibabu ya utapiamlo.
Kamati ilijadili pia uanzishwaji wa bustani ya mboga mboga katika shule zote za Wilaya ya Tunduru, na ilibainika kuwa kati ya shule 29 za Sekondari, ni shule 5 tu ambazo bado hazijafikiwa na programu hiyo. Hatua zilipendekezwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa bustani hizo zinawekwa katika shule zote.
Pichani: Baadhi ya wajumbe wa Kikao Cha kamati ya Lishe.
Afisa Lishe Wilaya ya Tunduru Bi. Martha Kibona alitolea ufafanuzi juu ya matumizi bora ya lishe ,hasa katika utumiaji wa chumvi yenye madini rutubishi kwa binadamu (Madini joto).
“Elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi juu ya matumizi bora ya chumvi hususani kuwa makini na Chumvi ambayo haina madini joto”. Alisema.
Pichani: kutoka kushoto ni Afisa Lishe Wilaya ya Tunduru Bi. Martha Kibona akiwa na Mwandishi wa vikao Bi. Laiti Zuberi.
Kamati iliazimia kuhakikisha upatikanaji wa mbegu za viazi lishe kwa umma na kuwahimiza wadau kusambaza mbegu hizo sehemu zote za Halmashauri. Hatua hii inalenga kuboresha upatikanaji wa chakula chenye lishe bora kwa jamii yote.
Kwa kipindi cha robo ya nne, Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Tunduru imezalisha maji na kusambaza kwa wateja Zaidi ya lita milioni 30 ambazo ni sawa na asilimia 50. Pia, imeendelea na kazi ya ukarabati na ujenzi wa miradi ya maji safi na salama Mjini Tunduru.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda,Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.