Kamati ya siasa ya Tunduru, chini ya uongozi wa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Mh.Abdalah A. Mtula, pamoja na mkuu wa wilaya ya Tunduru Mh. Julius Mtatiro, imefanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Tunduru. Habari njema ni kwamba miradi yote iliyokaguliwa imeonekana kuwa katika hatua nzuri ya utekelezaji.
Kamati hiyo ilifanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kusaidia kuimarisha maendeleo ya wilaya. Kamati ilishirikisha wataalamu na viongozi wa serikali katika ukaguzi huo ili kupata taarifa sahihi na kuweka mikakati ya kuendeleza miradi hiyo.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya na majengo ya afya. Kamati ilibaini kuwa miradi hiyo ilikuwa inatekelezwa kwa mujibu wa viwango na taratibu na ilikuwa na ufanisi mkubwa. Aidha, Kamati ilisifu juhudi za uongozi wa wilaya kwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi na kuhakikisha rasilimali zinapatikana kwa wakati.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ameelezea kuridhishwa na hatua iliyofikiwa na miradi ya maendeleo ya wilaya. Amesema miradi hii itaisaidia Wilaya ya Tunduru kuendelea kukua na kuboresha maisha ya wananchi wake. Pia, amewaasa viongozi na watendaji wengine kuendelea kusimamia na kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa.
“kazi yetu kubwa sisi ni kuangalia kile tulichowaagiza viongozi wetu wa serikali wametekeleza kwa kiasi gani, kazi ilingane na thamani ya fedha ambazo serikali imetoa”, Mh. Abdalah Mtula.
“sasa hivi kuna mradi wa bilioni 150 wa umeme ambao utatembea kilomita 250 kutoka Songea kuja mpaka hapa Tunduru na utamaliza kabisa tatizo la umeme katika wilaya yetu, hii inaonyesha kwamba Dr. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamua kupigania maendeleo ya Tunduru”. Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mh. Julius Mtatiro.
Kamati ya siasa ya Tunduru inaendelea kufuatilia na kusimamia miradi mingine ya maendeleo katika wilaya hiyo. Inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati na inakuwa na manufaa kwa wananchi wote.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
25/08/2023.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.