Kikao cha kawaida cha Kamati ya Lishe Wilaya kwa robo ya nne (Aprili-Juni) kimefanyika leo tarehe 29 Julai 2025, katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru. Lengo kuu la kikao hiki lilikuwa ni kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa masuala ya lishe kutoka idara na vitengo mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha hali ya lishe kwa wakazi wa Tunduru. Kikao kilihudhuriwa na wajumbe kutoka sekta muhimu zinazohusika na lishe, wakiwemo wataalam wa afya, kilimo, elimu, maendeleo ya jamii, RUWASA, na TUUWASA.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa kikao cha Kamati ya Lishe Wilaya ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Ndg. Chiza Marando alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za lishe wilayani. Alipongeza juhudi zilizofanywa katika robo iliyopita na kuwataka wajumbe kujadili kwa kina taarifa zitakazowasilishwa ili kubaini maeneo yenye mafanikio na yale yanayohitaji maboresho. Aliwakumbusha wajumbe kuwa lishe bora ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii na uchumi wa kaya, na hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya lishe bora.
Katika kikao hicho, idara na vitengo mbalimbali viliwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025. Idara ya Afya iliwasilisha taarifa kuhusu afya ya mama na mtoto, ikijumuisha viwango vya utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano na afya ya wajawazito,hata hivyo kulitolewa msisitizo kwa wananchi kujitahidi kuzingatia lishe bora ikiwa ni pamoja na kula vyakula vinavyoongeza damu mwilini. Idara ya Kilimo iliainisha juhudi za kuhamasisha kilimo cha mazao yanayostahimili ukame na yenye virutubisho vingi, huku Idara ya Elimu ikieleza programu za elimu ya lishe mashuleni. Vitengo vingine vilijadili masuala kama vile upatikanaji wa maji safi na salama, usafi wa mazingira, na programu za kuwajengea uwezo wanawake na vijana kiuchumi ili kuongeza kipato na kuboresha upatikanaji wa chakula.

Baada ya mawasilisho, kulikuwa na mjadala mpana ambapo wajumbe walichangia mawazo na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza. Baadhi ya changamoto zilizotajwa ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora, upatikanaji hafifu wa baadhi ya vyakula vya asili vilivyo na virutubisho, na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri uzalishaji wa chakula. Kamati ilisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa jamii, kuhamasisha matumizi ya bustani za mboga majumbani, na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na sekta binafsi katika masuala ya lishe.
Mwisho wa kikao, Kamati ya Lishe Wilaya ilikubaliana juu ya hatua madhubuti zitakazochukuliwa ili kuimarisha hali ya lishe wilayani Tunduru. Hizi ni pamoja na kuandaa mpango kazi wa kina kwa robo ijayo utakaozingatia mapendekezo yaliyotolewa, kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za lishe, na kutoa kipaumbele kwa maeneo yenye changamoto kubwa za lishe. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba Wilaya ya Tunduru inakuwa na wakazi wenye afya bora na wenye uwezo wa kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.