Tunduru 15/ 02/2020
Jumuiya ya wanyamapori NALIKA iliyopo katika wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma imekabidhi gawio kwa serikali lenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya elimu katika shule tatu za sekondari za Namwinyu, Matemanga na Ligunga.
Akisoma taarifa kwa mkuu wa wilaya kabla ya kukabidhi gawio, Mwenyekiti wa jumuiya ya uhifadhi wa wanyamapori ya NALIKA Ndg Said Masoud amesema kuwa jumuiya hiyo imekuwa ikitoa gawio kwa serikali kila mwaka ikiwa ni kuunga mkono shughuli za serikali katika maeneo yanayozunguka jumuiya hiyo, na kwa mwaka huu imepanga kutoa zaidi ya milioni 30 lakini imeanza na milioni 15 kwa shule tatu kila moja shilingi milini tano ikiwa ni kwa ajili ya kujenga hosteli katika shule zilizopo maeneo yanayozunguka jumuiya hiyo.
Akiongea na waandishi wa habari pamoja na wanajumuiya ya NALIKA, Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro amesema serikali ina wajibu wa kushirikiana na jumuiya uhifadhi wanyamapori ya Nalika katika kufanya doria katika maeneo ya Jumuiya hiyo ili kupambana na wahalifu wanaovamia maeneo hayo na kwamba wasisite kuomba msaada kutoka kwa serikali.
Pia Mhe. Julius Mtatiro ameitaka jumuiya hiyo kuwa na ubunifu katika kupanga mikakati ya kupata mapato ya kutosha badala ya kutegemea tuu chanzo kimoja na uwindaji na ufadhili kutoka kwa wahisani.
Alisema “jumuiya hii imeundwa mwaka 2003 ambapo mwaka 2023 itafikisha miaka 20 hivyo ni vyema kupanga mikakati endelevu ya kupata mapato nje ya shughuli ya uwindaji ikiwa ni pamoja na kujikita katika shughuli za kilimo kama kilimo cha Ufuta na Korosho ili kuweza kujiendesha”
Julius Mtatiro alisisitiza umuhimu wa kuwa na mipango ya muda mrefu ili kuepuka kuomba fedha kwa wahisani kila wakati “ nataka kuanza kuona uwekezaji wenu mkubwa kwenye mashamba ya korosho na ufuta hata katika vijiji vingine kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi ili kupata ardhi kwa bei nafuu, na sitaki kuona taasisi ambayo ni tegemezi kwa wahisani na nitafanya ufuatiliaji”
Julius Mtatiro ametoa maagizo kwa wakuu wa shule zote tatu yaani Ligunga, Namwinyu na Matemanga kuunda kamati za usimamizi na ufuatiliaji wa fedha hizo na kuhakikisha kuwa zinafanya kazi iliyokusudiwa kwa kuzingatia kipaumbele cha shule husika ili kumaliza changamoto zilizopo kwa sasa.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya alimazilia kwa kusema kwamba ni kweli mkakati wa wilaya ya Tunduru ni kujenga Hosteli katika shule zote za sekondari wilayani Tunduru ili kupunguza mdondoko wa wanafunzi na mimba mashuleni lakini, alisisitiza kipaumbele kutolewa kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuweza kupokea idadi ya wanafunzi wote walipangwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.