Mkuuu wa wilaya ya Tunduru Mhe.Juma Zuberi Homera ametoa siku sita (6) kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Chikunja kijiji cha Angalia kilichopo Tarafa ya Lukumble mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kuwa saruji iliyopelekwa katika kijiji hicho kwa ajili ya kujenga sakafu katika visima viwili vya maji inajengewa ili visima hivyo vifungwe pumpu na kutoa huduma kwa wananchi.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kitongoji hicho baada ya kufika kufanya ukaguzi katika shule ya msingi Chikunja na uchimbaji wa visima 2 vya maji vinavyochimbwa kupitia fedha za kuchochea maendeleo ya Jimbo kusini na taasisi ya H.U.C (HELP FOR UNDESERVED COMMUNITY).
Mkuu wa wilaya alisema “nimesikitishwa sana na utendaji kazi wa mwenyekiti wa kitongji hiki kwani serikali imeleta saruji lakini cha ajabu miezi inaendelea tuu kupita lakini hamfanyii kazi huku wanawake wanateseka kufata maji mtoni umbali mrefu huku shughuli nyingine zote za maendeleo zikisimama”
Niwakumbushe kuwa Mhe.Mbunge amechangia kwa kila kisima shilingi 650,000 ili kuendana na kauli mbiu ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani lakini kuna watu wachache wanaotaka kukwamisha jitihada zinazofanywa na serikali, hatutawavumilia kabisa.
Kwa upande mwingine mkuu wa wilaya ya Tunduru aliwaagiza wananchi wa kitongoji cha Chikunja kupanga mipango ya namna bora ya unzishwaji wa ujenzi wa zahanati kwa kuandaa benki tofali ili kupunguza kero ya kutembea umbali mrefu kufata huduma za afya, huku katika kijiji cha Azimio akiwataka kuweka mpango bora wa usimamizi wa mazao ili kuweza kupata mapato yatakayotumika katika shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Azimio.
Mkuu wa wilaya huyo alisema "wananchi wa kitongoji hiki wanasafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 20 kufata huduma za afya katika kituo cha afya Mtina, ili kukabiliana na changamoto hii kijiji mama Angalia wameshafyatua tofali 2500 kwa aili ya ujenzi wa zahanati na nyie wanachikunja mfyatue tofali ili serikali ione na kuwaletea vifaa vya kiwandani"
Aidha aliwataka wahudumu wa afya katika zahanati ya kijiji cha Azimio kutuoa huduma stahiki kwa wananchi kwani walipwa kupitia kodi za wananchi, ratiba ya utoaji huduma itolewe na ibandikwe katika mbao za ofisi za kijiji ili kuondoa usumbufu kwa wnanchi hasa siku za mapumziko na mwisho wa wiki.
Halmshauri ya Tunduru inaendelea kusimamia na kutekeleza kazi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma stahiki na kwa wakati, kwa wananchi wanaokumbana na changamoto msisite kutoa taarifa kwa serikali.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.