Siku ya wanawake duniani ilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900, kupitia wanawake waliokuwa wanafanya kazi katika sekta ya viwanda nchini Marekani walioandamana kupinga mazingira duni ya kazi zao, wakilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira. Kutokana na hali hiyo nchi ya Marekani iliridhia kuwa na siku kitaifa ambayo itakuwa kwa ajili ya kujadili na kuridhia masuala mbalimbali yanayohusu wanawake.
Baadaye Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa mwaka 1945, ilipofika tarehe 8 Machi iliridhiwa iwe siku ya kimataifa ya wanawake duniani. Uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa ulitokana na kukubali kwake kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake yanahitaji msukumo maalum na wa pekee.
Madhumuni ya maadhimisho ilikuwa ni kumuonesha upendo na heshima mwanamke kutokana na mafanikio yake katika nyanja mbalimbali kama vile siasa, kijamii na kiuchumi. Ni siku ambayo wanawake hutambuliwa kutokana na mafanikio yao bila kujali mgawanyiko wa itikadi za utaifa, ukabila, lugha, utamaduni, uchumi au siasa.
Katika taifa la Tanzania maadhimisho ya sikukuu ya wanawake duniani imeanza kuadhimishwa mnao mwaka 1996, maadhimisho yamekuwa yakiandaliwa kitaifa na katika ngazi ya mkoa na wilaya.
Kimsingi Tanzania imepiga hatua tangu kuanza kuadhimisha siku ya wanawake duniani, kwani kumekuwa na mwamko mkubwa wa wanawake kushiriki katika maendeleo na ngazi za uamuzi ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Ukweli ni kwamba, awali wanawake wengi walikuwa wakihofia hata kuwania nafasi kubwa za kisiasa kama vile urais, ubunge na nafasi nyingine za kiutendaji kutokana na hofu ya kutopewa nafasi.
Kwa mfano kwa miaka zaidi ya 40, ushiriki wa wanawake bungeni ulikuwa haufiki asilimia 20. Taarifa zinaonesha kuanzia mwaka 1961 hadi 1965 ushiriki wa wanawake bungeni ulikuwa ni asilimia 1.9 wakati wanaume ilikuwa asilimia 98.1. Mwaka 1965 hadi 1970 wanawake ushiriki wao ulikuwa asilimia 4.0 wakati wanaume, mwaka 1970 hadi 1975 asilimia 4.0, mwaka 1975 hadi 1980 asilimia7.3, mwaka 1980 hadi 1985 asilimia 10, 1985 hadi 1990 asilimia 10 na mwaka 1990 hadi 1995 asilimia 18.
Hivi sasa kutokana na harakati mbalimbali ikiwemo mikakati inayowekwa katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, hali imebadilika na idadi ya ushiriki wa wanawake katika chombo hicho kwa sasa inafikia takribani asilimia 22. Hata vinyang’anyiro vya nafasi za juu za uongozi, wanawake wameanza kujitokeza kuwania. Mwaka 2005, ndipo mwanamke wa kwanza aliandika historia ya kuwania urais. Alikuwa Dk Anna Senkoro (sasa marehemu) aliwania kupitia chama cha PPT-Maendeleo.
Baada ya hapo, wanawake wengine waliojitokeza ni Anna Mghwira wa ACT-Maendeleo aliyeingia kwenye kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Wanawake wengine waliowania nafasi hiyo katika ngazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Asha- Rose Migiro na Amina Said.
katika ngazi ya kitaifa tumeona jinsi wanawake wameweza kujitokeza na kusimama katika nafasi za juu kisiasa lakini pia katika bazara la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Tunduru taarifa imetanabaisha kuwa katika chaguzi za nyumba baraza la madiwani halikuwa na uchache wa wanawake kujitokeza kuwania nafasi za udiwani.
Taarifa zinaonesha kuwa mwaka 2010 katika baraza la madiwani lilikuwa na asilimia 25.5 ya wanawake, na mwaka 2015 ongezeko la asilimia 28.6 ya wanawake.
Tanzania ni miongoni mwa jamii ya kimataifa ambayo kila mwaka hushiriki katika maadhimisho ya sikukuu ya wanawake duniani katika ngazi ya kitaifa hadi wilaya. Mwaka 2018 katika Halmashauri ya Tunduru iliyopo mkoani Ruvuma maadhimisho haya yatafanyika katika Tarafa ya Nakapanya kijiji cha Nakapanya.
Maadhimisho haya yatatanguliwa na maandamano ya wanawake wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali za kuhamasisha maendeleo ya mwanamke. Watafika katika gezera la majimaji kuwatembea wafungwa kwani ni miongoni mwa watu ambao wamepoteza matumaini ili kuonesha upendo na pia kufika katika kituo cha afya Nakapanya kuwatembelea wagonjwa.
Katika siku hiyo ya kilele wanawake watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kupitia hotuba kutoka kwa viongozi wa kisiasa za kuhamasisha maendeleo ya wanawake na njia za kujikwamua kiuchumi. Hundi yenye thamani ya shilingi milioni 27 kutoka mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo la Tunduru Kaskazini zitatolewa kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali.
Hundi hiyo inatarajiwa kukabidhiwa na Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Ruvuma Bi Jackline Msongosi kwa vikundi vya wananwake kutoka katika Vijiji na Kata za jimbo la Tunduru Kaskazini ikiwa ni muendelezo wa jitihada za serikali kumkomboa mwanamke kiuchumi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.