Wilaya ya Tunduru leo imeonesha umoja na mshikamano wa hali ya juu kupitia harambee ya kuchangia ujenzi wa Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tunduru, iliyofanyika katika Ukumbi wa Skyway, Tunduru Mjini.
Harambee hiyo imewakutanisha viongozi wa chama, wabunge, madiwani na wanachama kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya chama na kuongeza ufanisi wa utendaji wake. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Denis Masanja, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, na kupongeza mshikamano uliooneshwa na wanachama wa CCM Tunduru.

Pichani:Mhe.Denis Masanja, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru akizungumza katika Harambee.
Kupitia harambee hiyo, jumla ya Tshs. 106,055,000/- zimekusanywa pamoja na mifuko 15 ya saruji, ambapo Tshs. 28,300,000/- ni fedha taslimu na Tshs. 77,755,000/- ni ahadi. Kiasi hicho kinaonesha dhamira ya dhati ya viongozi na wanachama wa CCM katika kuhakikisha ujenzi wa ofisi hiyo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili, ili iwe kituo imara cha kuratibu shughuli za chama wilayani.

Miongoni mwa waliochangia ni Madiwani wa CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru waliotoa jumla ya Tshs. 25,000,000/-. Wengine ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Ndugu Salim Abri (Asas) aliyechangia Tshs. 5,000,000/- taslimu, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi ya CCM Mkoa wa Iringa, Ndugu Ahmed Asas aliyetoa Tshs. 3,000,000/- taslimu, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Mhe. Judith Kapinga na Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Mhe. Mhandisi Fadhil Chilombe, kila mmoja akichangia Tshs. 5,000,000/-.

Michango mingine imetolewa na Dkt. Juma Matindana na Ndugu Saleh Kazembe waliotoa Tshs. 5,000,000/- kila mmoja, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Juma Homera aliyechangia Tshs. 1,000,000/-, pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Mariam Nyoka aliyetoa Tshs. 1,500,000/-.

Pichani: Mhe:Abdallah Mtila, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tunduru.
Aidha, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tunduru, Ndugu Abdallah Mtila, amechangia Tshs. 500,000/- taslimu na kuwashukuru wote kwa moyo wao wa kujitolea. Harambee hiyo imeacha ujumbe mzito kuwa mshikamano na ushirikiano wa wanachama na viongozi ni nguzo muhimu ya kuijenga CCM imara na kuisukuma Tunduru mbele kimaendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.