Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imefanya kikao cha kawaida cha kujadili utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe Februari 5, 2024.
Kikao kiliongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe, Adv. Julius S. Mtatiro na kilihudhuriwa na Watendaji Kata na Wakuu wa idara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru..
Katika kikao hicho, Mwenyekiti aliwataka watendaji katika kata kuzidi kurekebisha viashiria vya chini vya lishe katika jamii, alitilia mkazo umuhimu wa watoa huduma za afya kutembelea kaya zenye wajawazito na watoto chini ya miaka mitano mara kwa mara ili kuwapa elimu ya lishe bora na kufuatilia afya zao.
“ kwa ushirikiano wa viongozi , watendaji na wadau wote, lishe bora itaweza kupatikana kwa wananchi wote wa wilaya ya Tunduru”
Taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe iliwasilishwa na kaimu Afisa Lishe wa Wilaya Ndg. Martin Kigosi. Taarifa hiyo ilionyesha kuwa kata ya Matemanga imefanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa mkataba huo. Kwa mafanikio haya, kata ya Matemanga ilipewa cheti cha pongezi na zawadi ya pesa kiasi cha shilingi laki moja.
Wakizungumza katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe walipendekeza mikakati mbalimbali ya kuboresha lishe katika wilaya ya Tunduru. Mikakati hiyo ni pamoja na, Kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayofanya kazi katika sekta ya lishe, Kuanzisha bustani za mboga mboga katika kaya na shule na Kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora
Mwenyekiti wa kikao alihitimisha kikao hicho kwa kuwashukuru wajumbe wote kwa ushiriki wao na kuwataka waendelee kutekeleza majukumu yao kwa bidii ili kuboresha lishe katika wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.