Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mh. Wakili, Julius S. Mtatiro, amepongeza mradi wa Kiuma wa Kilimo kwa kuanza kutoa mafunzo ya miaka miwili kwa vijana ili kuwawezesha kujiajiri na kuajiri wengine.
Mradi wa Kiuma wa Kilimo umeanzishwa na Taasisi ya Kiuma chini ya ufadhili wa kampuni ya kijerumani iitwayo Deichmann Company kwa lengo la kutoa Elimu biashara na kusaidia vijana wa Wilaya ya Tunduru kujikwamua kiuchumi. Mpaka sasa kwa mwaka wa kwanza wa masomo 2023/2024 vijana 42 wanaendelea kupata mafunzo.
Mradi wa Kiuma wa Kilimo unatoa mafunzo ya vitendo kwa vijana, mafunzo haya hutolewa kwa miaka miwili. Katika mwaka wa kwanza wanajifunza zaidi kilimo cha mboga mboga ambacho wanaangalia mahitaji ya mboga mboga ambazo zinazosaidia sana kuongeza lishe na virutubisho kwenye mwili wa Mwanadamu, na mafunzo ya ufugaji hutolewa mwaka wa pili wa mafunzo hayo.
“Nimevutiwa sana na mradi huu. Ni mradi wa kipekee ambao una lengo la kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi. Ninaunga mkono mradi huu na nitatoa ushirikiano wa kutosha ili uweze kufanikiwa kwa ubora”. Alisema Mh. Mtatiro.
Pichani ( mwenye kofia Nyeusi): DC Mtatiro akizungumza katika ukaguzi wa Mradi wa Kiuma wa Kilimo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu Mkuu wa Taasisi ya kilimo Kiuma ndugu, Daniel Malukuta alisema mradi huo ni wa kipekee na una uwezo wa kuinua uchumi wa vijana na nchi kwa ujumla. Ambapo, wameandaa vitalu nyumba( Green House) kwa ajili ya kilimo hicho, kilimo cha umwagiliaji na usindikaji wa chakula.
“tumeona ni bora hawa vijana tuwachukue tuwaweka hapa ili tuwape mafunzo na kuwajengea uwezo wa kuzalisha mazao mbalimbali ambayo yatawasaidia katika biashara na kuwapa ujuzi wa kufuga wanyama na samaki ili kuwapatia kipato kutokana na mahitaji ya uko mtaani”. Alisema
Alisema,katika shamba la kujifunzia kwa vitendo wameanza kuzalisha kabichi,nyanya,pilipili,bilinganya,karoti,vitunguu na bamia na katika hatua ya kwanza, vijana wanafundishwa namna ya kuandaa shamba,matuta na vitalu nyumba(green House)ambapo kupitia njia hiyo mkulima anaweza kutumia eneo dogo la uzalishaji na akilihudumia vizuri atapata mazao na mapato mengi.
Vile vile, vijana wanafundishwa kutengeneza mbolea ya mboji(asili) ambayo inatengenezwa kwa kutumia mabaki ya mimea,nyasi,mashudu ya alizeti na samadi inayochanganywa na udongo na pia mbolea ya asili ina faida nyingi kwenye uzalishaji ikiwemo kumpunguzia mkulima gharama ambayo upatikanaji wake unahitaji fedha nyingi na kusababisha baadhi ya wakulima kushindwa kumudu gharama.
Mradi wa Kiuma wa Kilimo ni mfano wa jinsi ya kutumia kilimo na ufugaji kusaidia vijana kujikwamua kiuchumi. Mradi huo unatoa fursa nzuri kwa vijana kujifunza ujuzi muhimu ambao unaweza kuwasaidia kuanzisha kilimo biashara wenyewe. Ambapo unatarajiwa kuwawezesha kujiajiri na kupunguza idadi kubwa ya vijana wasiokuwa na ajira Wilayani Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.