Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe.Julius S. Mtatiro, amewataka Watendaji na viongozi ngazi ya kata na kijiji kuonesha ushirikiano wa karibu kwa Makarani wanaouhuisha na kusajili taarifa za Wakulima wa korosho.
Ametoa wito huo katika kikao kazi kilichowahusisha maafisa tarafa, Watendaji wa kata, maafisa kilimo, viongozi na Watendaji wa vyama vya Msingi vya ushirika na chama kikuu cha ushirika Tunduru pamoja na baadhi ya wakulima.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Bodi ya Korosho tawi la Tunduru, Bi. Shauri Mokiwa, amesema lengo la kikao hicho ni kuendelea kutoa msisitizo kwa viongozi na Watendaji ngazi ya serikali katika kata na vijiji kusimamia kwa ukaribu zoezi la uhuhuishaji na usajili wa Wakulima wa korosho wilaya ya Tunduru.
Aidha, Mhe. Mtatiro ameitaka Bodi ya Korosho Tanzania kuendeleza zoezi hili mpaka Machi 31, 2024 kutokana na ukubwa wa eneo la Wilaya ya Tunduru ukilinganisha na maeneo jirani ambapo zoezi hili linafanyika pia. amewataka Wakulima wa korosho kuonesha ushirikiano na kujitokeza kwa wingi ili kukamilisha zoezi hilo kwa wakati.
“Uchumi wetu ni mazao , hususani zao la korosho, tushirikiane katika kutimiza zoezi hili ”. Alisema Mhe. Mtatiro
Sambamba na hayo, DC Mtatiro amevipongeza vyama vya Ushirika vya Msingi na Chama kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) kwa kuonesha utendaji kazi mzuri, pia ameviomba kuwa mabalozi wa zoezi hili kwa wakulima katika maeneo yao husika.
Wilaya ya Tunduru inakadiliwa kuwa na zaidi ya Kilometa za Mraba 18,000 ,ambapo shughuli kubwa ni kilimo hasa zao la korosho, ambapo kwa msimu uliopita Wilaya ya Tunduru ilifanikiwa kukusanya zaidi ya Tani 25,000 za Korosho.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.